Rais wa Uturuki, ameadhimisha miaka 103 tangu kuanzishwa kwa Jamhuri ya Uturukk, akisisitiza maendeleo ya nchi hiyo katika sekta ya ulinzi, na diplomasia.
Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan, amesema kuwa nchi yake inaendelea kudumisha utulivu huku ikichukua nafasi ya kusaidia kutafuta suluhu ya migogoro, katika kipindi ambacho vita, machafuko na changamoto mbalimbali zinaendelea kushuhudiwa katika maeneo ya jirani na sehemu nyingine za dunia.
Erdogan alitoa kauli hiyo katika ujumbe wa video uliotolewa Siku ya Jamhuri ya Uturuki, inayoadhimishwa tarehe 29 Oktoba. Katika ujumbe huo, aliwapongeza wananchi wa Uturuki, Waturuki wa Kupro pamoja na raia wa nchi hiyo wanaoishi ughaibuni kwa kusherehekea siku hiyo muhimu ya kitaifa.
Pia alitumia salamu wageni waliokuwa katika ofisi za kidiplomasia za Uturuki na watu wanaoshiriki uhusiano wa kihistoria na kitamaduni na nchi hiyo, akiwatambua kwa kushirikiana na Waturuki katika nyakati za furaha na huzuni.
Rais Erdoğan alisema Jamhuri ya Uturuki ni ushahidi mkubwa wa dhamira ya taifa hilo ya kuishi kwa uhuru, kulinda mamlaka yake ya kujitawala na kuamua mustakabali wake bila kuingiliwa na wengine.
Alibainisha kuwa mapambano ya ukombozi yaliyoongozwa na Mustafa Kemal Atatürk, mwanzilishi wa Jamhuri ya Uturuki, yalidhihirisha uwezo wa taifa lililoungana kufikia malengo yake hata linapokabiliwa na mazingira magumu zaidi.
Mapambano ya ukombozi na uhuru wa taifa
Erdogan alisema mafanikio yaliyopatikana licha ya vikwazo na rasilimali chache yalibadilisha mwelekeo wa historia ya taifa hilo, huku yakithibitisha nguvu ya dhamira ya wananchi na haki yao ya kuishi kwa uhuru.
Alisisitiza kuwa Uturuki itaendelea kuzingatia misingi ya amani na haki, kwa kuongozwa na kaulimbiu yake isemayo, “Amani nyumbani, amani duniani.”
Erdogan amesema, ujasiri na dhamira iliyoonyeshwa na taifa hilo miaka 103 iliyopita bado ni chanzo cha msukumo kwa Uturuki ya sasa.
Alitaja maendeleo yaliyopatikana katika kipindi cha miaka 24 iliyopita, hususan katika sekta za ulinzi, nishati, usafiri na diplomasia, akisema hatua hizo zimekuwa nguzo muhimu katika juhudi za kuifanya Uturuki kuwa nchi yenye ushawishi mkubwa zaidi na ustawi mpana.
Erdogan alieleza kuwa serikali inaendelea kuwekeza katika teknolojia zinazozalishwa nchini, kupanua uwezo wa sekta ya ulinzi, kuimarisha usalama wa upatikanaji wa nishati, kuboresha miundombinu ya usafiri na kuongeza uwezo wa uzalishaji wa taifa.
Dira ya Uturuki ya siku zijazo
Akizungumzia mustakabali wa nchi hiyo, Erdogan alisema Uturuki yenye wakazi milioni 86 ina dhamira ya kutekeleza kwa vitendo dira yake ya “Karne ya Uturuki”, inayolenga kuiongoza nchi hiyo katika hatua mpya ya maendeleo na mafanikio.
“Kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu, Uturuki ina nguvu zaidi leo kuliko ilivyokuwa jana. Mungu akipenda, kesho itakuwa na nguvu zaidi, itaheshimiwa zaidi na kuwa na ushawishi mkubwa zaidi katika kila nyanja,” alisema Erdogan.
Aliongeza kuwa taifa la Uturuki lina azma ya kuweka alama yake katika karne hii kupitia maendeleo na nafasi yake katika masuala ya kimataifa.
Katika kuhitimisha ujumbe wake, Erdogan aliwakumbuka Atatürk, wapiganaji wenzake, mashujaa walioshiriki mapambano ya ukombozi na wote waliopoteza maisha yao wakilitetea taifa. Pia aliwashukuru na kuwaenzi maveterani walioshiriki katika kulitumikia na kulilinda nchi yao.
“Nawatakia heri ya maadhimisho ya miaka 103 tangu kuanzishwa kwa Jamhuri yetu,” alisema.

