Maadhimisho ya Oktoba 29 yanaashiria kuanzishwa kwa Jamhuri mwaka 1923, huku Rais wa Uturuki Erdogan akizungumzia kuhusu maendeleo ya nchi katika ulinzi, nishati, uchukuzi na diplomasia.
Uturuki inaadhimisha miaka 103 ya kuanzishwa kwa Jamhuri huku sherehe zikiendelea katika maeneo mbalimbali ya nchi.
Sherehe katika mji mkuu wa Ankara zimeanza kwa Rais Recep Tayyip Erdogan na maafisa waandamizi wa serikali wakitembelea kaburi la baba wa taifa Mustafa Kemal Ataturk.
Rais Erdogan ameweka shada la maua, na kukaa kimya kwa dakika moja na kusaini kitabu cha kumbukumbu, na baadae kupokea salamu za pongezi akiwa Ikulu.
Katika ujumbe alioutoa kwa njia ya video, Erdogan amesema Uturuki ina nguvu leo kuliko jana na itakuwa na nguvu zaidi, itafanikiwa na kuwa na ufanisi katika kila sekta katika siku za baadae. Pia amegusia kupiga hatua katika kipindi cha miaka 24 katika ulinzi, nishati, uchukuzi na diplomasia.
Jamhuri ilitangazwa Oktoba 29, 1923, huku wabunge wote 158 waliokuwepo bungeni wakiunga mkono. Ataturk baadae alichaguliwa kwa kura 158 kuwa rais wa kwanza.
Siku ya Alhamisi, maafisa waandamizi wa Uturuki pia waliadhimisha siku hiyo.
Waziri wa Katiba Akin Gurlek amesema serikali inafanyia kazi dira ya mwaka 2053 na 2071 chini ya uongozi wa Erdogan, ikilenga kufikia malengo makubwa zaidi, huku kiongozi wa Chama cha Nationalist Movement Party (MHP) Devlet Bahceli akisema chama chake kina azimia kubeba dira ya Jamhuri kuelekea "Karne ya Jamhuri."
Mkuu wa Shirika la Kijajusi la Taifa (MIT) Ibrahim Kalin amesema Jamhuri ni uhuru, umoja na mustakbali wa pamoja, na kuongeza kuwa MIT itaendelea kulinda usalama wa taifa na uhuru wa mipaka.
Viongozi wa nchi zinazozungumza Kituruki mjini Ankara
Sherehe za mwaka huu zinaenda sambamba na mkutano wa 13 wa Jumuia ya Nchi za Kiturk (OTS), ambao unaleta pamoja jijini Ankara viongozi wa nchi tano wanachama kuanzia Oktoba 29 hadi 30.
Erdogan atafungua Bustani la Kitaifa la Bestepe kwa onesho la wapanda farasi, baadae ataandaa chakula rasmi cha jioni kwa ajili ya viongozi waliofika.
Sherehe nchi nzima
Sherehe za Siku ya Jamhuri zinafanyika katika maeneo yote ya Uturuki.
Mpango wa "Turkiye Pedals" unawakutanisha waendesha baiskeli kutoka mikoa yote 81 kuanzia Oktoba 29 hadi Novemba 1, kuelekea mkutano wa COP31 utakaofanyika katika mji wa Antalya kuanzia Novemba 9 hadi 20. Watakaoshiriki uendeshaji huo wa baiskeli ni pamoja na wanariadha wenye leseni, vilabu vya baiskeli, wanafunzi, familia na wapenzi wa baiskeli. Lengo lake ni kuhamasisha matumizi ya baiskelti kama njia endelevu ya usafiri na kuongeza uelewa wa umma kuhusu mabadiliko ya tabianchi.

