Misheni hiyo itasitisha shughuli zake kwa mujibu wa maazimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na kufuatia ombi kutoka kwa serikali ya Somalia.
Misheni ya Umoja wa Mataifa nchini Somalia (UNTMIS) utahitimisha rasmi shughuli zake Oktoba 31, na hivyo kumaliza kipindi cha mpito cha miaka miwili pamoja na zaidi ya miongo mitatu ya misheni za Umoja wa Mataifa zilizokuwa zikisaidia juhudi za kuweka amani, kuimarisha utawala na kujenga taasisi za dola nchini humo. Hayo yamesemwa na afisa wa Umoja wa Mataifa Jumatatu.
Katika taarifa yake, msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, Stephane Dujarric, alisema kuwa misheni hiyo itasitisha shughuli zake kwa mujibu wa maazimio ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na kufuatia ombi la Serikali ya Somalia.
“Hatua hii muhimu inahitimisha zaidi ya miongo mitatu ya misheni ya Umoja wa Mataifa iliokuwa ikisaidia juhudi za kuweka amani, kujenga taasisi za dola, kuimarisha utawala na kukuza juhudi za maridhiano nchini Somalia,” alisema Dujarric.
Kufungwa huko kunafuatia mpango wa mpito uliyokubaliwa kwa pamoja, ambapo majukumu yaliyopewa UNTMIS yamehamishiwa kwa taasisi za Somalia, mashirika, mifuko na programu za Umoja wa Mataifa.
Umoja wa Mataifa kuendelea kutoa msaada
Dujarric alisema Guterres amesisitiza kuwa Umoja wa Mataifa utaendelea kuisaidia Somalia kupitia mashirika na programu zake zilizopo nchini humo, kwa kushirikiana na mamlaka za Somalia, Umoja wa Afrika na washirika wengine wa kimataifa, katika kuendeleza amani, utulivu, haki za binadamu na maendeleo endelevu.
“Kwa kutambua changamoto kubwa za kisiasa, kiusalama, kibinadamu na kimaendeleo ambazo bado zinaikabili Somalia, Katibu Mkuu anatoa wito wa kuendelezwa kwa msaada wa kimataifa ili kuimarisha mafanikio yaliyofanikishwa, kuendeleza mazungumzo ya kisiasa jumuishi na maridhiano, kuimarisha taasisi na kuimarisha pamoja na kulinda haki za binadamu,” aliongeza Dujarric.
Dujarric alisisitiza kuwa Guterres amethibitisha tena dhamira ya Umoja wa Mataifa ya kuendelea kuwasaidia wananchi wa Somalia na juhudi zinazoongozwa na Wasomali wenyewe za kujenga mustakabali wenye amani, utulivu na ustawi.

