Tukio hili limeongeza uchunguzi kuhusu vibali vya ujenzi, utekelezaji wa sheria na uwajibikaji wa wakandarasi na wataalamu wanaohusika katika miradi ya majengo marefu jijini Nairobi.

Serikali yazindua uchunguzi wa pamoja kuhusu chanzo cha kuanguka kwa jengo jijini Nairobi

Uchunguzi umeanzishwa kuhusu chanzo cha kuanguka kwa jengo katika mji mkuu wa Kenya, Nairobi siku ya Ijumaa huku maafisa wa kaunti wakitoa onyo kuhusu mijengo yote katika jiji.

Waziri wa Mambo ya Ndani Kipchumba Murkomen ametangaza uchunguzi wa pamoja utakaohusisha mashirika mengi ikiwa ni pamoja na huduma ya polisi ya kitaifa, idara ya uchunguzi wa jinai DCI, idara ya ukaguzi wa serikali ya kaunti na mamlaka ya ujenzi ya kitaifa.

Ripoti ya hivi karibuni kutoka kwa mashirika ya habari nchini Kenya inaonyesha kwamba watu saba bado hawajulikani walipo kufuatia kuanguka kwa jengo la ghorofa nyingi lililokuwa linaendelea kujengwa ingawa hakuna takwimu rasmi zilizotolewa huku shughuli za utafutaji na uokoaji zikiendelea.

Wakati huo huo Waziri wa Mambo ya Ndani Kipchumba Murkomen anasema wafanyakazi 67 wa ujenzi walikuwa kwenye eneo hilo wakati jengo hilo lilipoanguka. Sitini na sita waliponea bila kujeruhiwa na mmoja alijeruhiwa.

Watu saba walioripotiwa kupotea wanaaminika kuwa katika maduka 11 yaliyokuwa kwenye ghorofa ya chini na ya chini ya ardhi. Timu za uokoaji zimeripotiwa kuwasiliana na baadhi ya wale walionaswa kwenye jengo hilo.

Gavana wa Nairobi Johnson Sakaja ameibua wasiwasi kuhusu utekelezaji wa kanuni za ujenzi, akisema jengo lililoanguka lilikuwa limepokea idhini ya ujenzi lakini halikuwa na cheti cha lazima cha utumiaji.

''Hili linazua maswali kuhusu jinsi majengo hayo yalivyoruhusiwa kukaliwa, ikiwa ni pamoja na maduka kwenye ghorofa ya chini,'' alisema. ''Kutakuwa na msako wa jiji lote kuhusu maendeleo haramu na majengo yote yasiyofuata sheria yatakabiliwa na hatua za utekelezaji.'' Sakaja aliongeza.

Chanzo cha kuanguka bado hakijulikani. Tukio hilo limeongeza uchunguzi wa vibali vya ujenzi, utekelezaji wa sheria na uwajibikaji wa watengenezaji na wataalamu wanaohusika katika miradi mirefu jijini Nairobi.

Mnamo Januari mwaka huu, jengo lingine la ghorofa 12 lilianguka jijini Nairobi na kuua watu wasiopungua 2.

#