Meli hiyo ilikuwa na abiria 44 wa mataifa mbalimbali, wakiwemo raia 23 wa Msumbiji, 15 wa Tanzania, wanne wa Malawi na wawili wa Lesotho.

Watu watatu wamefariki baada ya meli kuteketea katika Ziwa Nyasa

Watu 40 wameokolewa baada ya meli ya abiria na mizigo kuungua moto na kuzama katika Ziwa Nyasa (linalojulikana pia kama Ziwa Malawi) mapema Jumapili, tukio lililosababisha vifo vya watu watatu.

Meli hiyo iliyosajiliwa nchini Msumbiji, MV Chambo, ilikuwa ikisafiri kutoka Mbamba Bay mkoani Ruvuma, Tanzania, kuelekea Metangula nchini Msumbiji wakati ajali hiyo ilipotokea.

Meli hiyo ilikuwa na abiria 44 wa mataifa mbalimbali, wakiwemo raia 23 wa Msumbiji, 15 wa Tanzania, wanne wa Malawi na wawili wa Lesotho.

Pia ilikuwa ikisafirisha takriban tani 10 za mizigo, ikiwemo mapipa ya petroli na dizeli yaliyokuwa yamepangwa kwenye sitaha ya wazi.

Uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa moto ulianzia kwenye sitaha na kuenea kwa kasi katika meli hiyo kabla ya kuzama. Taarifa za awali zinaonyesha kuwepo kwa hofu kuwa huenda sigara iliyotupwa ovyo ilisababisha kuwaka kwa mizigo hiyo inayoshika moto kwa urahisi.

Wavuvi wa eneo hilo wanaotumia boti zenye injini waliungana na timu za uokoaji katika kuwaokoa manusura kutoka majini.

Mamlaka zinatarajiwa kuchunguza chanzo cha moto huo huku taarifa zaidi zikiendelea kupatikana kuhusu mazingira yaliyozunguka ajali hiyo.

Meli hiyo, MV Chambo, ina uwezo wa kisheria kubeba hadi abiria 100 na tani 10 za mizigo. Pia ina njia panda (ramp) ya mbele inayoiwezesha kubeba magari.

#