Maafisa wa afya katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DR Congo) wameanzisha majaribio ya chanjo mpya ya Ebola huku mapambano ya kudhibiti mlipuko wa ugonjwa huo, unaoenea kwa kasi, yakiendelea.

Idadi ya walioambukizwa Ebola DRC yazidi 10,000, juhudi za kudhibiti ugonjwa huo zaendelea

Idadi ya waliothibitishwa kuambukizwa ugonjwa wa Ebola katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imezidi 10,000, kwa mujibu wa takwimu za serikali zilizotolewa Jumanne. Ripoti ya hivi karibuni ya kutathmini ugonjwa huo, iliyotolewa na taasisi ya taifa inayohusika na afya ya umma, ilionyesha kuwa idadi ya wagonjwa imefikia 10,060.

Tangu nchi hiyo ilipotangaza mlipuko wake wa 17 wa Ebola mwezi Mei, zaidi ya watu 4,600 wamefariki dunia. Katika kipindi cha miaka 50 iliyopita, virusi vya Ebola vimesababisha vifo vya zaidi ya watu 15,000 barani Afrika.

Nchi jirani ya Uganda ilitangazwa kuwa hakuna tena maambukizi ya Ebola mwezi Agosti na Shirika la Afya Duniani (WHO), baada ya kurekodi maambukizi ya watu 20 na ugonjwa huo, huku wawili wakifariki dunia.

Maambukizi mingine yameripotiwa nchini Kenya, ambako watu wawili wamefariki dunia. Nigeria, ambayo ndiyo nchi yenye idadi kubwa zaidi ya watu barani Afrika, nayo iliripoti maambukizi yake ya kwanza ya Ebola. Mgonjwa huyo ni mwanamke aliyewasili katika mji mkuu wa nchi hiyo, Abuja, kwa ndege kutoka Uganda.

Wakati huohuo, maafisa wa afya nchini DRC walianzisha majaribio ya chanjo mpya ya Ebola Ijumaa iliyopita, huku juhudi za kudhibiti kuenea kwa kasi kwa ugonjwa huo zikiendelea, kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO).

Ofisi ya WHO Afrika ilisema kuwa washiriki wa kwanza katika majaribio hayo ya chanjo mpya, inayojulikana kwa jina la Tumaini, walipatiwa chanjo hiyo katika mji wa Bunia, makao makuu ya jimbo la Ituri.

Kwa mujibu wa WHO, majaribio hayo yanaendeshwa kwa kuzingatia viwango madhubuti vya kisayansi, uwazi, misingi ya maadili na ridhaa inayotolewa baada ya washiriki kuelewa taarifa muhimu kuhusu utafiti huo. Aidha, majaribio hayo yanahusisha ushirikishwaji wa jamii katika mchakato mzima.

#