Lissu alikamatwa mwezi Aprili 2025 baada ya kuhutubia mkutano uliotoa wito wa kufanyika kwa mageuzi ya uchaguzi kuelekea uchaguzi mkuu nchini Tanzania. Siku iliyofuata, alifunguliwa mashtaka ya uhaini.

Kiongozi wa upinzani nchini Tanzania, Tundu Lissu, ametishia kuanza mgomo wa kula kuanzia 26 Oktoba

Kiongozi wa upinzani nchini Tanzania, Tundu Lissu, ambaye anashikiliwa gerezani, amesema ataanza mgomo wa kula siku ya Jumatatu. Hatua hii inalenga kupinga kile ambacho wakili wake anakielezea kama kukataa kwa mamlaka kumruhusu kukutana kwa faragha na jopo lake la mawakili, licha ya kuwepo kwa amri ya mahakama.

Lissu, ambaye ni mwenyekiti wa chama kikuu cha upinzani, Chadema, amekuwa kizuizini kwa zaidi ya miezi 18 na anakabiliwa na shtaka la uhaini ambalo linaweza kuadhibiwa kwa hukumu ya kifo.

Wakili wake, Rugemeleza Nshala, anasema Lissu alimjulisha kuhusu mpango huo wa mgomo wa kula wakati wa ziara ya kumtembelea gerezani siku ya Jumamosi.

Nshala anasema alimuonya mteja wake kuhusu hatari za kiafya, hasa kwa kuwa Lissu anatumia dawa muhimu kwa afya yake, lakini kiongozi huyo wa upinzani alionyesha kuwa yuko tayari kuacha kuzitumia.

Lissu, ambaye alishika nafasi ya pili katika uchaguzi wa urais wa mwaka 2020, alikamatwa mwezi Aprili 2025 na kushtakiwa kwa uhaini kwa madai ya kuchochea umma kususia uchaguzi wa mwaka jana.

Tanzania imekuwa ikifuatiliwa kwa karibu kufuatia maandamano yaliyotokea wakati wa uchaguzi uliofanyika mwezi Oktoba, huku upinzani ukidai kuwa maelfu ya watu waliuawa.

Uchunguzi rasmi kuhusu vurugu zilizohusiana na uchaguzi huo ulibaini kuwa angalau watu 518 walipoteza maisha.

Lissu, ambaye alinusurika jaribio la mauaji mwaka 2017 ambapo alipigwa risasi mara 16, aliwahi pia kufanya mgomo wa kula mwezi Mei 2025 kupinga sharti la kuhudhuria vikao vya mahakama kwa njia ya mtandao.

Hukumu ya mwisho katika kesi yake ya uhaini imepangwa kutolewa tarehe 6 Novemba, 2026.

Hadi kufikia siku ya Jumamosi, mamlaka za magereza, polisi, na serikali ya Tanzania hazikuwa zimetoa tamko lolote hadharani kuhusu mpango huo wa mgomo wa kula.

#