Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Michezo (CAS) imebatilisha uamuzi wa Shirikisho la Soka Barani Afrika (CAF) wa kuitangaza Morocco mabingwa kufuatia vurugu wakati wa fainali za mwezi Januari.

Senegal yarudishiwa ubingwa wao wa AFCON 2025

Senegal wamerudishiwa ubingwa wao wa AFCON 2025 baada ya Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Michezo (CAS) siku ya Jumanne kukubali rufaa yao ya kupinga kupokonywa taji hilo.

Senegal ilipinga uamuzi wa Shirikisho la Soka la Afrika (CAF) wa kutangaza kuwa Morocco ndiyo mabingwa wa fainali hizo, licha ya Senegal kuwafunga wenyeji hao 1-0 katika mechi iliyochezwa mjini Rabat mwezi Januari.

Senegal iliondoka uwanjani kwa dakika 14 baada ya Morocco kupewa penati katika dakika za mwisho, huku wachezaji kadhaa wakirudi kwenye vyumba vya mapumziko kupinga uamuzi huo kabla ya kurudi na kuanza tena kucheza.

Morocco ilikosa penati hiyo, na kusababisha mechi kuendelea dakika za ziada, ambapo Senegal walifunga goli la ushindi na kuwa mabingwa wa fainali hiyo.

Kuondoka uwanjani

Hata hivyo, Senegal walivuliwa ubingwa miezi miwili baadaye pale Bodi ya Rufaa ya CAF ilipoamua kuwa walisusia mechi kutokana na kuondoka uwanjani, kupindua matokeo na kuwapa Morocco ushindi wa magoli 3-0.

Senegal iliwasilisha rufaa katika Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi ya Michezo (CAS), ambayo iliwasilishwa tarehe 25 Machi lakini ikasikilizwa Oktoba 8.

Jopo la CAS, lililoongozwa na mtaalamu wa sheria ya michezo Mfaransa Gerald Simon akisaidiwa na raia wa Italia profesa wa sheria ya kimataifa Luigi Fumagalli na Ulrich Haas, mwanasheria mwenye makao yake Hamburg na profesa wa sheria katika Chuo Kikuu cha Zurich, lilibaini kuwa "mwamuzi hakuvunja sheria yoyote", alisema katibu mkuu wa CAS Matthieu Reeb.

TRT Afrika Swahili — TRT Afrika Swahili

Picha: Reuters (Wi

#