Ndege hiyo ilituma kwa muda mfupi ishara ya dharura ya kabla ya kubadili na kutuma kodi ya hatari ndani ya ndege.

Ndege ya UAE yatua Saudi Arabia baada ya marubani kupigana angani

Ndege iliyokuwa ikisafiri kutoka Dubai kwenda Tel Aviv ililazimika kubadili njia na kutua Saudi Arabia baada ya marubani wake kuripotiwa kupigana wakiwa angani.

Ndege hiyo ilituma kwa muda mfupi ishara ya dharura, kabla ya kubadili na kutuma kodi inayotumika kuashiria hatari ndani ya ndege, ikiwa ni pamoja na uwezekano wa kutekwa kwa ndege.

Kwa mujibu wa gazeti la Israel la Ynet, mapigano kati ya marubani wa ndege hiyo ya abiria yalisababisha kutumwa kwa kodi ya utekaji wa ndege, kabla ya ndege hiyo kutua Saudi Arabia Jumatano.

Ynet iliripoti kuwa ndege hiyo ilipangwa kutua katika Uwanja wa Ndege wa Ben Gurion. Ilikuwa imewabeba abiria 174 na kwa muda mfupi ilituma ishara ya dharura.

Ndege hiyo iliendeshwa na shirika la ndege la flydubai lenye makao yake Dubai na ilikuwa njiani kutoka Dubai kwenda Tel Aviv wakati tukio hilo lilipotokea.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, kodi inayoashiria uwezekano wa kutekwa kwa ndege ilitumwa wakati wa mzozo uliotokea ndani ya chumba cha marubani.

Baadaye ndege hiyo ilitua katika Uwanja wa Ndege wa Tabuk nchini Saudi Arabia.

Takriban dakika 90 baada ya kuruka, wakati ndege hiyo ikiingia katika anga ya Jordan, ilituma kodi “7700”, ambao ni ishara ya kimataifa unaotumika kuashiria dharura, gazeti hilo lilisema.

Baadaye ilituma kodi “7500”, inayotumika kuashiria hatari katika ndege, ikiwa ni pamoja na uwezekano wa kutekwa.

Wakati huo huo, ndege hiyo ilibadili mwelekeo, kurejea katika anga ya Saudi Arabia na kuanza kuruka katika mwinuko wa chini juu ya nchi hiyo, kwa mujibu wa taarifa hiyo.

Baada ya awali kuelekea kusini, ndege hiyo iligeuka kuelekea magharibi huku ikiendelea kubaki ndani ya anga ya Saudi Arabia, kabla ya kutua nchini humo.

Nahodha na rubani msaidizi wajeruhiwa

Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Prince Sultan bin Abdulaziz mjini Tabuk ulisema katika taarifa kuwa Kituo chake cha Kudhibiti Usafiri wa Anga kilipokea simu ya dharura kutoka kwa ndege ya flydubai, FZ1073, saa 8:44 asubuhi ikiomba kutua kwa dharura.

Uwanja huo ulisema hali ya dharura ilitangazwa na maandalizi yakafanywa ili kuisaidia ndege hiyo, ambayo ilifanikiwa kutua salama.

Uwanja huo uliongeza kuwa nahodha wa ndege pamoja na rubani msaidizi walijeruhiwa na kupelekwa hospitalini kwa ajili ya matibabu.

Kuna taarifa zinazokinzana kuhusu uraia wa marubani hao wawili. Kituo cha televisheni cha Israel, Channel 12, kilisema wafanyakazi wa chumba cha marubani walikuwa rubani kutoka Urusi na rubani msaidizi kutoka Ukraine. Hata hivyo, Ynet iliripoti kuwa rubani anayeshukiwa kujaribu kuigongesha ndege hiyo ni raia wa Oman, huku rubani wa pili akiwa raia wa UAE.

Baadaye Channel 12 ilisema tukio hilo linaonekana kutokuwa na uhusiano na usalama, huku mamlaka zikichunguza iwapo ishara ya dharura ilitumwa kwa bahati mbaya kutokana na mabishano kati ya nahodha na rubani msaidizi.

Baadaye shirika la ndege liliwaarifu mamlaka za Israel kuwa ndege nyingine ingetumwa kutoka Dubai kwenda Saudi Arabia ili kuwarejesha abiria wa Israel waliokuwa kwenye ndege hiyo, Ynet iliripoti.

Mamlaka ya Viwanja vya Ndege ya Israel, kwa upande wake, ilikanusha taarifa kwamba anga ya nchi hiyo ilikuwa imefungwa wakati wa tukio hilo.

Hata hivyo, maafisa waandamizi katika sekta ya usafiri wa anga nchini Israel walisema uwezekano wa tukio la kiusalama kwenye ndege hiyo ya flydubai bado haujaondolewa, kwa mujibu wa Ynet.

Kwa mujibu wa tathmini ya awali iliyonukuliwa na maafisa hao, mmoja wa marubani alidaiwa “kujaribu kuisababisha ndege hiyo ianguke,” lakini rubani mwingine alifanikiwa kuzuia jaribio hilo kwa msaada wa baadhi ya abiria wa Israel.

Ofisi ya Waziri Mkuu wa Israel ilisema hali hiyo ilikuwa “inadhibitiwa” na kwamba “njia zote zinatumika kwa sasa kuhakikisha abiria wa Israel wanarejeshwa salama nchini Israel.”

#