Rais wa Uturuki ametoa wito wa kusitishwa mara moja kwa vita, huku akiahidi kuwa Uturuki itaendelea kuunga mkono juhudi za amani katika eneo hilo, katika mkutano uliofanyika pembezoni mwa COP31.

Erdogan ataka kusitishwa kwa vita vya Marekani dhidi ya Iran, katika mkutano wake na Pezeshkian

Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan, ametoa wito wa kusitishwa mara moja kwa vita vinavyoendelea kati ya Marekani na Iran, akisisitiza umuhimu wa kurejea katika meza ya mazungumzo ya kidiplomasia ili kumaliza mzozo huo bila kuchelewa.

Erdogan alitoa wito huo siku ya Alhamisi, Novemba 12, 2026, alipokutana na Rais wa Iran, Masoud Pezeshkian, pembezoni mwa mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu mabadiliko ya tabianchi (COP31), uliofanyika katika jiji la Antalya, kusini mwa Uturuki.

Katika mazungumzo hayo, Erdogan alisisitiza kuwa pande zinazohusika zinapaswa kurejea katika meza ya mazungumzo, huku akieleza kuwa Uturuki itaendelea kuunga mkono juhudi za kidiplomasia zinazolenga kurejesha amani na utulivu katika eneo hilo.

Erdogan amesema kuwa: “Ni muhimu kuimarisha maeneo yanayoweza kuwaunganisha wadau katika kufikia makubaliano na kuipa diplomasia kipaumbele.”

Pia alieleza matumaini yake kuwa vita hivyo vitamalizika haraka iwezekanavyo, akiahidi kuwa Uturuki itaendelea kushirikiana na nchi za eneo hilo katika juhudi za kutafuta suluhu ya amani.

Vita vyazua hofu kuhusu athari kwa mazingira

Vita hivyo vilianza Februari 28, kufuatia mashambulizi ya Marekani na Israel dhidi ya Iran, yaliyosababisha kifo cha Kiongozi Mkuu wa Iran, Ali Khamenei.

Iran ilijibu mashambulizi hayo kwa kurusha makombora na ndege zisizo na rubani dhidi ya maeneo mbalimbali katika ukanda huo. Wakati huohuo, makundi yanayoungwa mkono na Tehran nchini Lebanon, Yemen na Iraq nayo yaliingia katika mzozo huo.

Akizungumza katika mkutano wa COP31 siku ya Jumatano, Rais Pezeshkian aliishutumu Marekani na Israel kwa kusababisha uharibifu mkubwa wa mazingira kupitia mashambulizi yao dhidi ya Iran.

Pezeshkian amesema: “Uchokozi wa hivi karibuni, ambao ni wa kihalifu na kinyume cha sheria, uliofanywa dhidi ya Iran na Marekani pamoja na utawala wa Kizayuni... umesababisha uharibifu mkubwa wa mazingira, huku ukisababisha kiasi kikubwa cha uchafuzi wa mazingira na gesi zinazochangia ongezeko la joto duniani.”

Wakati huo huo, juhudi za kidiplomasia zinazoongozwa na Qatar na Pakistan zimeendelea kwa lengo la kutafuta makubaliano yatakayomaliza vita hivyo.

Kwa upande wake, Iran inaitaka Marekani ikubali masharti kadhaa, yakiwemo kuondoa zuio la mali za Iran zilizozuiwa pamoja na kuondoa vikwazo vya kiuchumi vilivyowekwa dhidi ya nchi hiyo.

Masharti hayo yanatolewa huku Iran ikihusisha utekelezaji wake na kufunguliwa tena kwa Mlango-Bahari wa Hormuz, njia muhimu ya kimataifa inayotumiwa kusafirisha nishati, ambayo Iran imeifunga tangu kuanza kwa vita hivyo.

TRT Afrika / TRT World and Agencies — TRT Afrika / TRT World and Agencies

Picha: Anadolu Agency (Wire)

#