Mke wa Rais wa Uturuki anasema kuwa mpango huo utaleta nchi pamoja ili kuendeleza miradi ya pamoja; kauli hiyo imetolewa wakati akiandaa mkutano wa ngazi ya juu wa wake wa viongozi, pembezoni mwa mkutano wa COP31 unaofanyika Antalya.

Muungano wa Kutokomeza Taka kugeuza suluhisho za ndani kuwa hatua za kimataifa: Emine Erdogan

Mke wa Rais wa Uturuki, Emine Erdogan, amesema kuwa Muungano wa Kimataifa wa Kutokomeza Taka utaziunganisha nchi mbalimbali kwa lengo la kubadilishana uzoefu na mbinu bora, kuanzisha miradi ya pamoja na kuendeleza suluhisho zinazozingatia mzunguko wa uchumi.

Kauli hiyo aliitoa alipokuwa mwenyeji wa mkutano wa ngazi ya juu uliowakutanisha wake na wenza wa viongozi wa dunia, pembezoni mwa mkutano wa COP31 uliofanyika mjini Antalya.

Emine Erdogan amezindua Muungano wa Kimataifa wa Kutokomeza Taka (Global Zero Waste Alliance) katika mkutano wa COP31, akitoa wito wa kuimarishwa kwa ushirikiano wa kimataifa ili wajibu wa pamoja wa kulinda mazingira ugeuzwe kuwa ushirikiano wa kudumu na hatua madhubuti.

Akizungumza Jumatano katika mkutano huo aliouandaa mjini Antalya, pembezoni mwa mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu mabadiliko ya tabianchi, Emine Erdogan alisema kuwa muungano huo utatoa fursa kwa nchi mbalimbali kubadilishana uzoefu na mbinu zilizofanikiwa, kuanzisha miradi ya pamoja na kusambaza suluhisho zilizobuniwa katika ngazi za ndani ili zitumike duniani kote.

Alisema kuwa muungano huo unaonesha dhamira ya pamoja ya kuvuka hatua ya kutoa ahadi na kuhakikisha kuwa uelewa kuhusu masuala ya mazingira unazaa matokeo yanayoonekana.

"Muungano wa Kimataifa wa Kutokomeza Taka tunaouanzisha leo unaonesha dhamira yetu ya kuugeuza wajibu huu wa pamoja kuwa ushirikiano wa kudumu," alisema.

Emine Erdogan, ambaye ni mwenyekiti wa Bodi ya Washauri wa Watu Mashuhuri kuhusu Kutokomeza Taka ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, alisisitiza kuwa dunia inapaswa kuacha kujikita katika kujadili vitisho vya mabadiliko ya tabianchi na badala yake kuelekeza nguvu katika utekelezaji wa suluhisho.

"Ni wakati sasa wa kuvuka hatua ya kutegemea ripoti, maonyo na malengo yanayoonesha ukubwa wa janga la tabianchi," alisema.

Aliongeza kuwa thamani ya maarifa inapaswa pia kupimwa kwa kuzingatia maamuzi na hatua zinazochochewa na maarifa hayo.

Aliutaja mkutano wa COP31 kuwa ni "COP ya Utekelezaji wa Hatua" (Action COP), akisema Uturuki inataka mafanikio ya mkutano huo yasipimwe kwa ahadi zinazotolewa pekee, bali pia kwa mabadiliko yanayoletwa katika maisha ya watu, miji na mifumo ya uzalishaji.

Akizungumzia Mpango wa Kutokomeza Taka wa Uturuki (Zero Waste Movement), ulioanzishwa miaka tisa iliyopita, Emine Erdogan alisema kuwa mpango huo umekua kutoka katika juhudi za kuhamasisha kaya kuhusu utunzaji wa mazingira na kuwa mfumo wa kitaifa unaohusisha shule, halmashauri, taasisi za umma na viwanda.

Alibainisha kuwa kiwango cha uchakataji taka nchini Uturuki kimeongezeka kutoka asilimia 13 hadi zaidi ya asilimia 37 katika kipindi hicho, huku uwajibikaji wa kimazingira ukizidi kuwa sehemu ya maisha ya kila siku.

Wito wa uwajibikaji mkubwa zaidi kwa makampuni

Akizungumzia maendeleo ya teknolojia, Emine Erdogan alisema kuwa akili unde (AI) ina fursa kubwa za kusaidia kupunguza taka, kuongeza ufanisi katika uzalishaji na kubuni suluhisho za kukabiliana na changamoto za mazingira.

Hata hivyo, alionya kuwa maendeleo ya teknolojia hayapaswi kutenganishwa na gharama zake kwa mazingira.

"Hatuwezi kujenga teknolojia za siku zijazo kwa kutegemea mazoea ya ubadhirifu ya zamani," alisema.

Alitoa wito wa kuwepo kwa viwango vya pamoja vya kimataifa vitakavyohakikisha kuwa makampuni makubwa yanaweka wazi kiasi cha rasilimali wanazotumia, yanafanyiwa tathmini huru kuhusu athari za shughuli zao kwa mazingira na kuimarisha uwajibikaji.

"Wajibu wa makampuni yanayofanya shughuli zake katika kiwango cha kimataifa nao unapaswa kuwa wa kimataifa," aliongeza.

Emine Erdogan pia alizungumzia madhara makubwa ya kimazingira yanayosababishwa na migogoro ya kivita, akisema kuwa vita husababisha uharibifu wa mazingira ambao athari zake zinaweza kudumu kwa vizazi vingi.

Akizungumzia Gaza, alinukuu makadirio ya Mpango wa Mazingira wa Umoja wa Mataifa (UNEP) yanayoonesha kuwa tani milioni 61 za vifusi zimekusanyika katika eneo hilo la Palestina. Aidha, asilimia 97 ya bustani za matunda na mashamba ya mizeituni yameharibiwa, huku sehemu kubwa ya vyanzo vya maji safi vilivyosalia vikiwa vimechafuliwa.

Alionya kuwa kurejesha hali ya mazingira katika maeneo yaliyoharibiwa kunaweza kuchukua vizazi kadhaa.

Wakati matumizi ya kijeshi duniani yakifikia kiwango cha rekodi cha dola trilioni 2.9, Emine Erdogan aliitaka jumuiya ya kimataifa kutafakari kile ambacho kingeweza kufanikishwa iwapo hata sehemu ndogo ya fedha hizo ingeelekezwa katika kukabiliana na changamoto za pamoja za kibinadamu na kimazingira.

"Miji ingeweza kujengwa upya, maeneo ya ardhi yaliyoharibiwa kurejeshwa katika hali nzuri, na amani ingekuwa hali ya kawaida katika kila bara," alisema.

Maeneo matano ya kipaumbele ya muungano huo

Emine Erdogan alisema kuwa Muungano wa Kimataifa wa Kutokomeza Taka utajikita katika maeneo matano ya kipaumbele ambayo ni: kutokomeza taka na kuendeleza mzunguko wa uchumi ; taka za plastiki na vifungashio; maeneo yasiyozalisha taka; taka za chakula na taka za kikaboni; pamoja na elimu na vijana.

Alisema kuwa muungano huo pia utafanya kazi kupitia mifumo mitatu inayokamilishana, ikiwemo Jukwaa la Mwaka la Kutokomeza Taka (Zero Waste Forum), litakalotumika kujadili vipaumbele na suluhisho za pamoja.

Mfumo mwingine ni Jukwaa la Istanbul (Istanbul Platform), litakalosaidia kubadilisha mapendekezo kuwa miradi na ushirikiano unaotekelezeka.

Alisema kuwa muungano huo utalenga kuwakutanisha mashirika ya kimataifa, mamlaka za serikali za mitaa, taasisi za elimu ya juu, sekta binafsi na asasi za kiraia ili kushirikiana katika kufikia malengo ya pamoja.

Akisisitiza kuwa hakuna nchi inayoweza kukabiliana na changamoto za mazingira peke yake, Emine Erdogan aliwaalika wake na wenza wa viongozi waliohudhuria mkutano huo kuwa washirika hai wa mpango huo na kushirikisha uzoefu pamoja na mbinu zilizofanikiwa katika nchi zao.

Alisema kuwa mkutano huo unapaswa kufungua njia ya kuanzishwa kwa ushirikiano mpya, miradi ya pamoja na maendeleo yanayoweza kupimika. Aliwahimiza washiriki kurejea katika nchi zao wakiwa na dhamira ya kuendeleza ushirikiano huo.

Mkutano huo uliwakutanisha wake na wenza wa viongozi mbalimbali wa dunia, wakiwemo Janja Lula da Silva wa Brazil, Ziroat Mirziyoyeva wa Uzbekistan, Ancelly Simina wa Micronesia, Sajidha Mohamed wa Maldives na Gueta Selemane Chapo wa Msumbiji.

Washiriki wengine walikuwa Nilden Bektaş Erhürman, mke wa Rais wa Jamhuri ya Kituruki ya Kupro ya Kaskazini; Francine Ntakarutimana wa Burundi; Zubaida Rahman, mke wa Waziri Mkuu wa Bangladesh; pamoja na Zainab Suleman, mkwe wa Waziri Mkuu wa Pakistan.

Mkuu wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), Alexander De Croo, na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Makazi ya Watu (UN-Habitat), Anacláudia Rossbach, pia walihutubia mkutano huo.

TRT Afrika / TRT World and Agencies — TRT Afrika / TRT World and Agencies

Picha: َAA

#