Nchi hizo tatu za Sahel zilijiondoa rasmi kutoka ECOWAS mnamo Januari 2025.

Burkina Faso, Niger na Mali zarejelea mazungumzo na ECOWAS

Burkina Faso, Niger na Mali zimeanza tena mazungumzo na jumuiya ya kikanda ya Afrika Magharibi, ECOWAS, ambayo ziliijiondoa zaidi ya miezi 18 iliyopita, huku zikikubaliana kushirikiana kuelekea uundaji wa "mkataba wa mfumo" wa ushirikiano.

Nchi hizo tatu ziliondoka katika Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika Magharibi (ECOWAS) mnamo Januari 2025, baada ya kuungana na kuunda kundi lao wenyewe, linalojulikana kama Muungano wa Nchi za Sahel (AES).

Mazungumzo kati ya ECOWAS na AES yalikuwa yakiendelea tangu Januari 2025, lakini siku ya Jumamosi yalifanyika kwa mara ya kwanza katika ngazi rasmi ya mawaziri.

‘Ujirani mwema’

Katika taarifa ya pamoja iliyotolewa Jumamosi jioni, pande zote mbili "zilipongeza roho ya udugu, kuheshimiana na uwazi" iliyojitokeza katika mazungumzo hayo, na kusisitiza umuhimu wa kudumisha uhusiano wa "ujirani mwema", hasa kwa kuzingatia "heshima kwa mamlaka ya kujitawala".

Zilikubaliana "kuunda vikundi kazi vya pamoja vya kisekta ili kufikia mkataba wa mfumo wa ushirikiano".

Ujumbe wa AES uliongozwa na Karamoko Jean-Marie Traore, Waziri wa Mambo ya Nje wa Burkina Faso, huku ujumbe wa ECOWAS ukiongozwa na Cheikh Niang, mwenzake kutoka Senegal.

Nchi wanachama wa AES zimekata uhusiano na Ufaransa, ambayo ilikuwa nchi ya kikoloni hapo awali, na kwa upanuzi huo, zimekata uhusiano pia na nchi kadhaa katika eneo hilo ambazo zinaziona kuwa na uhusiano wa karibu mno na Paris; hatua hii inafanyika huku nchi hizo zikifuata dira ya kupinga ukoloni mamboleo na kutetea mamlaka kamili ya kujitawala.

#