Kwa namna ya pekee, amewataka viongozi wa dini kumuombea Rais Samia apate wasaidizi waaminifu na wakweli na waendelee kumuomba Mungu afunge mageti ya ikulu dhidi ya 'watu wabaya'.

Tanzania: Dkt. Nchimbi awaomba viongozi wa dini kumuombea Rais Samia

Makamu wa Rais wa Tanzania, Emmanuel Nchimbi amewaomba viongozi wa dini kuendelea kumuombea Rais Samia Suluhu dhidi ya watu wabaya ili wasipate nafasi ya kumsogelea yeye mwenyewe na Ikulu.

Dkt. Nchimbi  amewataka viongozi wa dini nchini humo, kumuombea afya njema,busara na hekima rais wa taifa hilo, Samia Suluhu Hassan. kwa kuwa ndiye kiongozi Mkuu wa Nchi na kupitia yeye nchi itaendelea kuwa salama.

Kwa namna ya pekee, amewataka viongozi wa dini kumuombea Rais Samia apate wasaidizi waaminifu na wakweli na waendelee kumuomba Mungu afunge mageti ya ikulu dhidi ya ‘watu wabaya’.

“Watu wenye mawazo mabaya waone Ikulu hapaingiliki kwa namna yoyote ile. Wasitamani hata kusogea karibu na rais,” alisema Dkt. Nchimbi wakati wa wa hafla ya kusimikwa Uongozi wa Kitaifa wa Awamu ya Tano wa Baraza la Makanisa ya Kipentekoste Tanzania (CPTC), iliyofanyika Februari 6, 2026 jijini Dar es Salaam.

Hali kadhalika, makamu huyo wa Rais wa Tanzania, alitoa wito kwa viongozi hao kuhamasisha waumini kulinda mazingira kwa kuepuka ukataji miti, uchomaji misitu na uharibifu wa vyanzo vya maji, huku wakichochea upandaji miti kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.

Katika kuimarisha ushirikiano wa Serikali na taasisi za dini, alibainisha kuwa Rais Samia ametoa hekari 12 Dodoma kwa ajili ya makao makuu ya CPTC pamoja na shilingi milioni 100 kuanza ujenzi. Aidha, aliwashukuru wadau wa dini kwa mchango wao katika elimu, afya na malezi ya jamii, huku akiahidi Serikali kuendelea kulinda amani ya Taifa.

Comments

Comment

Comment Your email address will not be published. Required fields are marked*

No comments Yet

#