Maafisa wanasema makubaliano hayo ya viza, pamoja na mipango ya ndege za mojakwa moja kati ya mataifa hayo mawili yataimarisha biashara, utalii, na masuala ya elimu.

Somalia na Tanzania yakubaliana kuhusu ziara bila viza, na kupata viza mtu anapowasili

Somalia na Tanzania wamesaini makubaliano ya uhamiaji yanayoruhusu raia wa nchi hizo mbili kuingia nchini bila ya viza na pia kupata viza wanapowasili, hatua inayotarajiwa kuimarisha biashara, utalii, na masuala ya elimu.

Makubaliano hayo yalitiwa saini na Waziri wa Mambo ya Ndani wa Somalia Abdullahi Sheikh Ismail Fartaag, pamoja na Waziri wa Mambo ya Ndani wa Tanzania Patrobas Paschal Katambi.

Pia katika hafla hiyo alikuwepo Kamishna Jenerali wa Uhamiaji wa Tanzania Anna P. Makakala, Mkurugenzi Mkuu wa Uhamiaji wa Somalia Mustafa Sheikh Ali Dhuhulow, na balozi wa Somalia nchini Tanzania Ilyas Ali Hassan.

 Makubaliano ya ushirikiano

Makubaliano hayo yanaimarisha makubaliano ya awali kati ya mataifa hayo mawili, ikiwemo yale ya usalama, kuhusu kubadilishana wafungwa, na yale ya kuimarisha lugha ya Kiswahili na utamaduni. Makubaliano mengine ni ushirikiano wa kisiasa, ulinzi, afya, na utalii.

Somalia, ambayo hivi karibuni iljiunga na Jumuiya ya Afrika Mashariki, imeimarisha ushirikiano na Tanzania katika miaka ya hivi karibuni.

Rais Hassan Sheikh Mohamud alitembelea Tanzania kwa mikutano kadhaa ya ngazi ya juu, ikiwemo katika sherehe za kuapishwa kwa Rais Samia Suluhu Hassan mwezi Novemba 2025. Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania Mahmoud Thabit Kombo alifanya ziara mjini Mogadishu mwezi Disemba 2024, na kukutana na maafisa wa Somalia kwa majadiliano kuhusu ushirikiano.

Maafisa wanasema makubaliano hayo ya viza, pamoja na mipango ya ndege za moja kwa moja kati ya nchi hizo mbili, yataimarisha biashara, utalii, na masuala ya elimu.

Comments

Comment

Comment Your email address will not be published. Required fields are marked*

No comments Yet

#