Mariam Abu Dagga, aliyeuawa katika shambulio la anga la Israel katika hospitali moja huko Gaza mwezi Agosti 2025, ameshinda tuzo hiyo pamoja na wenzake wawili kwa kuandika kwa kina madhara ya kibinadamu ya vita.
Mwandishi wa habari za vita wa Kipalestina, Mariam Abu Dagga, aliyeuawa katika shambulio la anga la Israel huko Gaza mwaka jana, ameshinda baada ya kifo chake tuzo ya hadhi ya Rory Peck kwa waandishi wa habari wa video wanaofanya kazi kwa kujitegemea, waandaaji wa tuzo hiyo wametangaza.
Abu Dagga ameshinda tuzo hiyo na wenzake wawili wa shirika la habari la Associated Press (AP), Abdel Kareem Hana na Jehad Alshrafi, waliotunukiwa "kwa uandishi wao wenye ujasiri kuhusu athari za vita hivyo kwa maisha ya umma" katika ardhi ya Palestina, kwa mujibu wa Taasisi ya Rory Peck (Rory Peck Trust).
Abu Dagga alikuwa na umri wa miaka 33 alipouawa Agosti 2025 wakati wa shambulio la anga la Israel lililolenga Hospitali ya Nasser kusini mwa Gaza. Shambulio hilo pia liliua waandishi wengine wanne wa habari.
Mpiga picha na mwandishi huyo wa video anayejitegemea alikuwa akiripoti pamoja na AP tangu kuanza kwa vita vya mauaji ya halaiki Oktoba 2023.
Mhariri mkuu wa AP, Julie Pace, alisema: "Waandishi wa habari wana nafasi muhimu katika kuweka kumbukumbu za matukio na kuujulisha umma, mara nyingi huku wakihatarisha maisha yao binafsi kwa kiwango kikubwa."
"Tunamuenzi Mariam na waandishi wote wa habari waliouawa katika mzozo huu na migogoro mingine, na tunaendelea kujitolea kutafuta majibu kuhusu vifo vyao."
Tuzo hizo za kila mwaka zilianzishwa mwaka 1995 kwa kumbukumbu ya Rory Peck, mwandishi wa habari wa video anayejitegemea aliyeuawa alipokuwa akiripoti mgogoro wa kikatiba mjini Moscow mwaka 1993. Zinatambua ujasiri, uhuru na mchango muhimu wa wakusanyaji habari wanaojitegemea kote duniani.
Chanzo: Taasisi ya Rory Peck (Rory Peck Trust) na Associated Press (AP).
TRT Afrika — TRT Afrika
Picha: AP

