Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki, Hakan Fidan, amesema kuwa msaada unaohitajika unatolewa kwa ajili ya kuilinda Saudi Arabia. Aidha, ametangaza uwezekano wa kufanyika kwa mkutano wa pili wa nchi za R4 na E4 mjini Berlin mwezi ujao.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki, Hakan Fidan, amesema kuwa sera ya Uturuki inaweka kipaumbele katika ulinzi wa Saudi Arabia, huku akithibitisha kuwa hakuna uamuzi ambao umefikiwa kuhusu kupeleka wanajeshi wa Uturuki nchini Yemen.
"Kwa sasa, sera yetu inalenga katika kuilinda Saudi Arabia. Hakuna uamuzi uliofanywa kuhusu kupeleka wanajeshi ndani ya Yemen. Hata hivyo, msaada unaohitajika kwa ajili ya kuilinda Saudi Arabia unatolewa," Fidan alisema hayo kwenye mahojiano na televisheni ya Uturuki ya TGRT Haber siku ya Jumamosi.
Akizungumzia ushirikiano katika sekta ya ulinzi kati ya Uturuki, Pakistan, Saudi Arabia na washirika wengine ambao wanaweza kujiunga baadaye, Fidan alisema kuwa ushirikiano huo ni moja ya nguzo kuu za Muungano wa Ulinzi wa Makkah.
Alibainisha kuwa Uturuki imewahi kukumbana na changamoto za kiusalama kutokana na baadhi ya washirika wake kuikatalia silaha, hali ambayo imeifanya nchi hiyo kutambua umuhimu wa ushirikiano wa pamoja katika sekta ya ulinzi.
Fidan alisema kuwa mkataba wa usalama wa Makkah haulengi nchi yoyote. Badala yake, alisema, nchi wanachama zinalenga kujenga suala la kuaminiana na kuimarisha ushirikiano mpana wa kiuchumi.
Alifafanua kuwa kifungu cha ulinzi wa pamoja kinachofanana na Ibara ya 5 ya mkataba wa NATO hakimaanishi kwamba hatua za kijeshi zitachukuliwa moja kwa moja kila tishio linapotokea. Badala yake, hatua hizo zinahitaji tathmini ya vitisho, ushirikiano wa kiintelijensia, mipango ya pamoja ya ulinzi na idhini ya Bunge la Uturuki.
Alisema utaratibu huo unafanana na ule unaotumika katika maamuzi ya kupeleka wanajeshi wa Uturuki nchini Syria, Iraq, Somalia, Lebanon na katika maeneo ya bahari ya kimataifa.
Akibainisha kuwa Saudi Arabia tayari inashirikiana na karibu nchi 30 kuhusu suala la Yemen, Fidan alisema mashambulizi ya mara kwa mara yaliyofanywa na Marekani, Uingereza na nchi za Ulaya dhidi ya wapiganaji wa Houthi hayajafanikiwa kukomesha vita nchini humo.
Hata hivyo, aliongeza kuwa mashambulizi ya Wahouthi katika Mlango-Bahari wa Bab el-Mandeb yameifanya Yemen kuwa suala la tishio kwa usalama wa dunia.
Diplomasia ya kuchukua hatua mapema na nafasi ya kushughulikia changamoto za eneo
Fidan alisema kuwa chini ya dira ya Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan, nchi hiyo imekuwa ikijenga mifumo ya kikanda yenye uwezo wa kufanya kazi kwa vitendo na kuleta ubunifu, badala ya kuanzisha miundo ya ushirikiano inayobaki kwenye matamko na ishara za kisiasa pekee.
Alitaja mifumo hiyo kuwa ni pamoja na Muungano wa Ulinzi wa Makkah, Muungano wa Nchi Nne wa Kikanda (R4), unaojumuisha Uturuki, Misri, Pakistan na Saudi Arabia, pamoja na kundi la nchi nane linalohusika na suala la Gaza (Gaza Group of Eight).
Alisisitiza kuwa kuchukua hatua za mapema katika maeneo muhimu ya kimkakati yanayobadilika kwa kasi, kabla migogoro haijazidi kuwa mikubwa, kumeisaidia Uturuki kuzuia misukosuko mikubwa ya kikanda na kimataifa yenye uwezo wa kutishia usalama na uwepo wake.
Kwa mujibu wa Fidan, hatua hizo zimeifanya Uturuki kuwa mdau ambaye mataifa mbalimbali yanamtafuta mara kwa mara kwa ajili ya mashauriano na kutafuta suluhu. Aliongeza kuwa dhana ya Uturuki ya eneo husika kuwa na nafasi ya msingi katika kuamua na kutafuta suluhu za changamoto za usalama na migogoro inayolikabili eneo lao, sasa inaanza pia kuungwa mkono na viongozi wa Ulaya.
Akielezea umuhimu wa majukwaa yasiyo rasmi na yasiyofungamana na maamuzi ya kisheria, Fidan alisema mifumo hiyo hurahisisha mazungumzo ya wazi bila vikwazo vya taratibu rasmi za kidiplomasia.
Alisema kuwa wakati Marekani inapunguza uwepo wake katika masuala ya usalama wa Ulaya kutokana na vita vya Urusi na Ukraine, Uturuki iliitisha mikutano ya makundi mawili mjini Istanbul: Muungano wa Nchi Nne za Ulaya (E4), unaojumuisha Ufaransa, Ujerumani, Italia na Uingereza, pamoja na Muungano wa Nchi Nne wa Kikanda (R4).
Fidan alisema kuna mipango ya kufanya mkutano wa pili wa makundi hayo mwezi ujao mjini Berlin, iwapo kila kitu kitaenda vizuri.
Aidha, Fidan alizungumzia pendekezo la Uturuki lililowasilishwa katika mkutano wa mawaziri wa mambo ya nje wa G20 uliofanyika nchini Marekani mwezi uliopita.
Alisema Uturuki ilipendekeza kupitishwa kwa tamko la kimataifa lenye nguvu ya kisheria litakalohakikisha kuwa usafirishaji wa kibiashara kupitia njia muhimu za baharini unaendelea bila kukatizwa, bila kujali kuwepo kwa vita au hali nyingine za kimataifa.
Njia hizo muhimu za baharini ni pamoja na Mlango-Bahari wa Hormuz, Mlango-Bahari wa Uturuki, Mlango-Bahari wa Gibraltar, Mlango-Bahari wa Malacca na Mfereji wa Panama.
Akionya kuhusu kuongezeka kwa mapigano katika Bahari Nyeusi, Fidan alisema hali hiyo inazidi kuhatarisha usalama wa meli za biashara.
Alisema meli zinashambuliwa karibu kila siku na kwamba Urusi pamoja na Ukraine zimetangaza kuwa zitalenga meli katika eneo hilo.
Fidan alieleza kuwa sambamba na tahadhari zinazotolewa na Wizara ya Uchukuzi ya Uturuki na Kamandi ya Jeshi la Wanamaji, nchi hiyo inaendelea kushirikiana na Urusi na Ukraine kupitia vyombo vyao vya ulinzi wa pwani na mamlaka za usafirishaji.
Aidha, alisema Uturuki imekuwa ikizihimiza meli zinazobeba raia wa Uturuki kujiepusha na maeneo yanayokumbwa na mapigano ili kulinda usalama wao.
TRT Afrika / AA — TRT Afrika / AA
Picha: AA

