Dollar

38,8394

-0.04 %

Euro

43,9430

-0.01 %

Gram Gold

4.116,5900

0.18 %

Quarter Gold

0,0000

%

Silver

0,0000

%

Ingawa baadhi wamekosowa hatua ya Rais Samia Suluhu wa Tanzania kuwatimua wanaharakati wa Kenya waliokwenda kushuhudia kesi ya Tundu Lissu, wengine wameipongeza

Baadhi wapongeza hatua ya Tanzania kuwatimua wanaharakati wa Kenya

Hatua ya serikali ya Tanzania ya kuwazuia baadhi ya wanaharakati kuingia nchini humo mwishoni mwa juma, huku wengine wakitimulia, kumeibua hisia tofauti miongoni mwa raia wa Kenya na Tanzania.

Wanaharakati na watumishi wengine wa umma walitaka kuhudhuria kesi ya kiongozi wa upinzani nchini Tanzania Tundu Lissu iliyokuwa katika mahakama moja jijini Dar es Salaam Mei 19.

Miongoni mwa waliorudishwa ni aliyekuwa waziri wa katiba na sheria Martha Karua, huku Jaji Mkuu mstaafu wa Kenya David Maraga, akiruhusiwa kuingia nchini Tanzania.

Mwanaharakati Boniface Mwangi alifanikiwa kuingia Tanzania lakini hakuweza kufika mahakama baada ya kukamatwa na maafisa wa usalama.

Hata hivyo, msimamo thabiti wa serikali ya Tanzania ulidhihirika pale rais Samia Suluhu Hassan, alipotoa kauli na kukemea vikali hatua ya baadhi ya wanaharakati kutoka Kenya kutaka kuingilia masuala ya ndani ya nchi yake.

Rais Samia, akionesha kutoridhishwa na hali hiyo, aliviagiza vyombo vya ulinzi na usalama, kuhakikisha kuwa wanachukua hatua madhubuti dhidi ya wanaharakati hao.

“Walishaharibu kwao, walishavuruga kwao, nchi iliyobaki haijaharibika, watu wako na usalama na amani na utulivu hapa kwetu.Niwaombe sana vyombo vya ulinzi na usalama, na nyingi wasimamizi wa sera zetu za nje kutokutoa nafasi kwa watovu wa adabu kutoka nchi nyengie kuja kutovuka hapa kwetu,” ameagiza Rais Samia.

Baadhi ya watu wameikosoa vikali kauli hiyo, ikiwemo Martha Karua, ambae ni mwanasheria na mwanasiasa, aliyedai kuwa, lengo la kuingia Tanzania halikuwa kuvamia nchi hiyo.

“Samia Suluhu, hatukuvamia nchi yako. Tumekuja kwa njia halali kama watu wa Afrika Mashariki (EAC), lakini tulizuiwa kuingia, kinyume na makubaliano ya kuingia,” alisema Karua.

Karua, mara kadhaa amejipata matatani kutokana na msimamo wake wa kutetea wapinzani wa serikali katika nchi za Afrika Mashariki kama vile suala la Kiiza Besigye wa Uganda. Pia kabla ya kurudishwa mwishoni mwa juma, aliwahi kuhudhuria kesi ya Lissu kama sehemu ya wanasheria wa upande wa utetezi.

David Maraga,  aliyekuwa Jaji Mkuu nchini Kenya, amelaani hatua hiyo ya kutimuliwa kwa baadhi ya wanaharakati kutoka Kenya akisema kuwa wao ni raia kutoka Jumuia ya Afrika Mashariki.

Hata hivyo, sio wote wanaopinga msimamo wa serikali ya Tanzania. Samson Cherargei, ambae ni seneta wa Kaunti ya Nandi, magharibi mwa Kenya, ameunga mkono hatua hiyo na kusema kuwa Rais Samia ana haki ya kuwazuia watu kutoka nje wanaoingilia masuala ya taifa lingine.

“Namuunga mkono kikamilifu Rais Suluhu kwa kuwapiga marufuku wanaharakati wa Kenya kutaka kuingilia masuala ya ndani ya nchi yake. Uhusiano wa kimataifa unataka kuwepo kwa heshima miongoni mwa mataifa rafiki,” amesema Cherargei.

Baadhi ya wananchi kutoka Kenya na Tanzania pia wameeleza kufurahishwa na kauli ya Rais Samia, ya kuwa na msimamo thabiti kwa nchi yake.

Wakati hayo yakijiri, mpaka sasa hatma ya wanaharakati Boniface Mwangi na Agather Atuhaire ambao wanadaiwa bado wamezuiliwa nchini Tanzania haijulikani huku kampeni zikiendelea mitandaoni za kutaka wawili hao waachiliwe huru.

Ikumbukwe kuwa, Bunge la Ulaya tayari limetoa kauli ya kutaka serikali ya Tanzania kumuachilia kiongozi huyo wa upinzani, Tundu Lissu hasa ikizingatiwa kwamba, imesalia miezi michache kabla ya Uchaguzi Mkuu wa nchi hiyo.

Serikali ya Tanzania imejibu kuhusu hayo na kusema kuwa, haina uwezo wa kuingilia mamlaka ya mahakama.

Comments

Comment

Comment Your email address will not be published. Required fields are marked*

No comments Yet

#