Sport
Dollar
43,2923
0.06 %Euro
50,7657
0.7 %Gram Gold
6.583,1300
1.33 %Quarter Gold
10.861,2400
0.91 %Silver
132,7900
1.18 %Ushindi wa Museveni unathibitisha nafasi yake kama mmoja wa viongozi wa Afrika wa muda mrefu, tangu kuingia madarakani mwaka 1986.
Viongozi mbalimbali wa Afrika wamejitokeza na kumpongeza rais mteule wa Uganda Yoweri Kaguta Museveni baada ya kutangazwa mshindi katika uchaguzi wa urais nchini humo. Huu utakuwa muhula wake wa saba madarakani.
Tume ya Uchaguzi ya Uganda ilisema Museveni, mwenye umri wa miaka 81, alipata asilimia 71.65 ya kura katika uchaguzi uliofanyika Alhamisi Januari 15, ambapo alimshinda mpinzani wake wa karibu, kiongozi wa upinzani Bobi Wine, aliyeipata asilimia 24.72.
Ushindi wa Museveni unathibitisha nafasi yake kama mmoja wa viongozi wa Afrika waliokuwepo madarakani kwa muda mrefu. Museveni aliingia madarakani kwa mara ya kwanza mwaka 1986.
Rais wa Rwanda Paul Kagame alikuwa miongoni mwa viongozi wa kwanza kumpongeza Museveni, huku akisifia ushirikiano endelevu kati ya nchi hizo mbili.
“Hongera, Rais @KagutaMuseveni kwa kuchaguliwa tena kuwa Rais wa Jamhuri ya Uganda,” Kagame alisema. “Nakupongeza wewe na watu wa Uganda mnapoendelea kuhudumia taifa lenu kwa ustawi wa watu wenu. Natarajia kuendelea kwa ushirikiano imara na wenye tija kati ya nchi zetu mbili.”
‘Uaminifu wa umma’
Nae Rais wa Kenya William Ruto alielezea ushindi wa Museveni kama tafsiri ya uaminifu wa umma kwa uongozi wake.
“Ushindi wako thabiti katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika hivi karibuni unaonyesha imani ambayo watu wa Jamhuri ya Uganda wanayo kwa uongozi wako binafsi na uaminifu unaoonekana kwa chama cha NRM,” Ruto alisema.
Rais wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud pia alimpongeza Museveni, akiiunganisha na utulivu wa kikanda.
“Chini ya uongozi wake, Uganda imepiga hatua za kuonekana katika maendeleo na utulivu wa kikanda,” alisema, na kuongeza kwamba Somalia “inasisitiza ahadi yake ya kuimarisha uhusiano wa ukaribu na Uganda.”
Kamisheni ya Umoja wa Afrika pia ilijiunga kwa pongezi, na Mwenyekiti wake, Mahmoud Ali Youssouf, akisifu jinsi uchaguzi ulivyofanyika.
‘Uhusiano wa pande mbili’
“Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika anasifu jinsi uchaguzi ulivyofanyika Uganda na anampongeza Mhe. Yoweri Kaguta Museveni kwa kuchaguliwa tena kwa 71.61% ya kura zilizopigwa,” AU ilisema katika taarifa baada ya uchaguzi wa Januari 15.
Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir aliuelezea ushindi wa Museveni kama “ushindi mkubwa” na kuonyesha hamu ya kuendelea kuimarisha uhusiano wa pande mbili.
“Watu wa Jamhuri ya Uganda wamekukabidhi tena uongozi kwa kukuchangua tena kwa muhula wa saba,” Kiir alisema. “Ninatarajia kufanya kazi kwa karibu nawe kukuza uhusiano wa pande mbili.”
Rais wa Misri Abdel Fattah el-Sisi pia alitoa pongezi zake
“Ninatoa pongezi zangu kwa kaka yangu na rafiki, Mheshimiwa Rais Yoweri Kaguta Museveni, wakati wa kuchaguliwa kwake tena,” el-Sisi alisema, akielezea matokeo kwamba yameonesha “imani ya watu wa Uganda kwa uongozi wake mwenye busara.”
Museveni mwenyewe alionesha msimamo thabiti baada ya kutangazwa mshindi, akisema matokeo yanaonyesha uungwaji mkono wa dhati wa chama chake licha ya idadi ndogo ya wapiga kura waliojitokeza. Kiwango cha asilimia 52 ni cha chini zaidi tangu Uganda irudishe mfumo wa vyama vingi mwaka 2006.
“Matokeo yanatoa taswira nzuri ya nguvu ya chama chetu. Upinzani wana bahati. Hawajawahi kuona nguvu yetu kamili,” Museveni alisema.
Hata hivyo, uchaguzi uligubikwa na utata. Mamlaka zilisitisha huduma za mtandao kwa siku kadhaa, wakati hitilafu za mashine za kutambua wapiga kura za bayometriki zilichelewesha zoezi la upigaji kura katika baadhi ya maeneo, ikiwa ni pamoja na mji mkuu Kampala.
Bobi Wine, mwenye umri wa miaka 43, mwanamuziki ambae baadae aliingia kwenye siasa, alisema aliamua kujificha baada ya vikosi vya usalama kuvamia nyumbani kwake mara baada ya kura.
Bobi Wine amepinga matokeo ya uchaguzi akidai ni batili kutokana na tuhuma za wizi wa kura, lakini serikali imekana tuhuma hizo na kumlaumu kwa kuhamasisha wafuasi wake kufanya vurugu.


Comments
No comments Yet
Comment