Zambia na Jamhuri ya Congo zajiondoa katika mashindano hayo, huku mwakilishi wa Zimbabwe, Roseanna Hall, akihangaika kupata viza ya kwenda Puerto Rico.

Vikwazo vya viza vyawazuia warembo wa Afrika kushiriki mashindano ya Miss Universe nchini Marekani

Vikwazo vya Marekani katika utoaji wa viza vimevuruga maandalizi ya mashindano ya mwaka huu ya kuwania taji la ‘Miss Universe'.

Zambia na Jamhuri ya Congo zimelazimika kuwaondoa wawakilishi wao katika mashindano hayo. Wakati huohuo, ushiriki wa Zimbabwe bado haujawa na uhakika, zikiwa zimesalia chini ya wiki mbili kabla ya fainali ya 'Miss Universe' kufanyika Puerto Rico.

Fainali ya toleo la 75 ya mashindano ya ‘Miss Universe’ inatarajiwa kufanyika Novemba 24, 2026, katika ukumbi wa José Miguel Agrelot Coliseum, jijini San Juan, Puerto Rico, eneo lililo chini ya mamlaka ya Marekani. Mashindano ya mwaka huu yanawakutanisha warembo kutoka zaidi ya nchi na maeneo 120 duniani.

Mwakilishi wa Zimbabwe, Roseanna Hall, amesema kupitia ujumbe aliouchapisha kwenye mtandao wa Instagram kuwa changamoto za kupata viza zimemzuia kusafiri kwenda Puerto Rico, licha ya kuwa amekuwa akijiandaa kwa mashindano hayo kwa miezi kadhaa.

Washiriki kutoka Sudan Kusini na Zimbabwe bado wanasubiri kupata viza zao.

"Kwa bahati mbaya, changamoto za kupata viza ya Marekani zimechelewesha safari yangu, lakini bado mapambano hayajaisha," aliandika Hall.

Amesema serikali ya Zimbabwe kwa kushirikiana na shirika linaloandaa ‘Miss Universe’ nchini humo zinaendelea na juhudi za kumsaidia kupata viza.

Wakati huohuo, shirika la ‘Miss Universe Zambia’ limetangaza kuwa mwakilishi wake, Pamela Mubanga, hatashiriki mashindano hayo kutokana na vikwazo vya Marekani vya viza.

Shirika hilo limesema uamuzi wa kujiondoa umetokana na vikwazo vilivyowekwa na serikali ya Marekani, wala si matatizo ya nyaraka za Mubanga au maandalizi yake ya mashindano.

Jamhuri ya Congo yapata mwakilishi wake wa kwanza

Nchini Jamhuri ya Congo, Georgina Kambongo aliandika historia baada ya kutangazwa kuwa mwakilishi wa kwanza wa nchi hiyo katika mashindano ya kuwania taji la ‘Miss World’.

Waandaaji wa mashindano hayo nchini humo wamesema kushindwa kwake kusafiri kwenda Puerto Rico kunatokana na vikwazo vya viza vilivyowekwa na Rais Donald Trump.

Kwa upande wa Sudan Kusini, waandaaji wamesema ushiriki wa mwakilishi wao, Adut Deng, bado haujawa na uhakika, licha ya juhudi za miezi kadhaa za kuhakikisha anapata nyaraka na vibali vinavyohitajika kwa safari hiyo.

"Sudan Kusini inastahili kuonekana, kusikilizwa na kuwakilishwa. Malkia wetu amebeba matumaini, ndoto, uzuri na uimara wa taifa," ilisema sehemu ya taarifa ya waandaaji.

Kwa mujibu wa tangazo la Rais wa Marekani, Donald Trump lililoanza kutekelezwa Januari 1, jumla ya nchi 19 zimewekewa vikwazo vya viza.

Vikwazo hivyo vinasitisha utoaji wa baadhi ya viza, zikiwemo visa ya matembezi, masomo, na uhamiaji wa kudumu kwa raia wa nchi zilizoathirika.

Fainali ya toleo la 75 ya mashidano ya ‘Miss World’ inatarajiwa kufanyika Novemba 24 jijini San Juan, mji mkuu wa Puerto Rico.

TRT Afrika and agencies — TRT Afrika and agencies

Picha: Wengine

#