Maafisa wa kutoa huduma za dharura wanawatafuta watu ambao huenda bado wako hai na wamenaswa chini ya kifusi. Tukio kama hilo limetokea wiki tatu zilizopita katika mji mkuu wa Kenya, Nairobi.
Watu sita wamefariki dunia na wengine watano kuokolewa baada ya jengo la ghorofa nane lililokuwa likijengwa kuporomoka katika eneo la Mlolongo, karibu na mji mkuu wa Kenya, Nairobi.
Tukio hilo limetokea Ijumaa, huku juhudi za uokoaji zikiendelea kuwatafuta watu wanaohofiwa kuwa chini ya kifusi cha jengo hilo.
Kwa mujibu wa maafisa wa kutoa huduma za dharura na uokoaji ya Kaunti ya Nairobi, watu watano waliokolewa wakiwa hai na kukikimbizwa hospitalini.
Eneo la Mlolongo, ambako jengo hilo liliporomoka, ni eneo lililopo takribani kilomita 20 kusini-mashariki mwa Nairobi.
Hata hivyo, bado haijabainika ni wafanyakazi wangapi waliokuwa katika eneo la ujenzi wakati jengo hilo lilipoporomoka.
Katika taarifa, maafisa wa uokoaji wamesema shughuli za uokoaji zinaendelea.
Wasiwasi kuhusu usalama wa ujenzi
Chanzo cha kuporomoka kwa jengo hilo bado hakijafahamika. Aidha, mamlaka hadi sasa hazijatoa majina ya watu waliofariki.
Tukio hilo limetokea wiki tatu baada ya jengo jingine la ghorofa 15 lililokuwa likijengwa kuporomoka katika eneo la Eastleigh jijini Nairobi, na kusababisha vifo vya watu wanane.
Matukio hayo mawili yameibua upya wasiwasi kuhusu usalama wa majengo nchini Kenya na namna kanuni za ujenzi zinavyotekelezwa.
Kumekuwa na wito kwa mamlaka kuimarisha ukaguzi wa majengo yanayojengwa, kuhakikisha viwango vya ujenzi vinafuatwa na kuwawajibisha waendelezaji wa miradi ya ujenzi wanaohusika na majengo yasiyokidhi masharti ya usalama.
TRT Afrika / AA — TRT Afrika / AA
Picha: X

