Hatua hiyo inaashiria kuanza kwa uchunguzi unaolenga kubaini wahusika na nafasi ya kila mmoja katika matukio hayo, huku tume ikiwataka wananchi na taasisi zenye taarifa au vielelezo vinavyoweza kusaidia uchunguzi kuviwasilisha.

Tanzania: Tume ya Jaji Lila yaanza kuchunguza waliopanga ghasia za Oktoba 29

Tume ya Rais ya Kuchunguza Matukio ya Wakati na Baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025, imeanza kuchunguza watu waliopanga, kufadhili, kuratibu na kushiriki katika ghasia zilizotokea kipindi hicho, baada ya kukamilisha uchunguzi wa awali kuhusu matumizi ya nguvu katika kudhibiti vurugu hizo.

Hatua hiyo inaashiria kuanza kwa uchunguzi unaolenga kubaini wahusika na nafasi ya kila mmoja katika matukio hayo, huku tume ikiwataka wananchi na taasisi zenye taarifa au vielelezo vinavyoweza kusaidia uchunguzi kuviwasilisha.

Mwenyekiti wa tume hiyo, Jaji Mstaafu Shaban Lila akizungumza na waandishi wa habari leo Jumanne, Oktoba 27, 2026 jijini Dar es Salaam, amesema tume imekamilisha ukusanyaji wa ushahidi katika wilaya zote za Mkoa wa Dar es Salaam na sasa imeanza kutekeleza hadidu ya rejea inayohusu kuwabaini waliohusika kupanga, kufadhili, kuratibu na kufanya ghasia wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025.

“Kwa upande wa Dar es Salaam, tume sasa imeanza kukusanya taarifa ambazo zitaiwezesha kutekeleza hadidu ya rejea namba moja, inayohusu kuwabaini wahusika katika kupanga, kufadhili, kuratibu na kufanya ghasia wakati ule wa uchaguzi mkuu wa mwezi Oktoba mwaka 2025,” amesema Jaji Lila.

Jaji Lila amesema kazi ya tume inaongozwa na hadidu za rejea zinazobainisha maeneo yanayopaswa kuchunguzwa, ikiwemo kubaini wahusika wa ghasia na kuchunguza malalamiko kuhusu namna vurugu zilivyodhibitiwa.

#