Tumerejea na sehemu nyingine ya mfululizo wetu unaoangazia vipaji vya riadha barani Afrika.

Jacob Kiplimo mashine kali ya Uganda inayonguruma katika mbio ndefu

Jacob Kiplimo alizaliwa katika Wilaya ya Kween, eneo la Mlima Elgon nchini Uganda, Novemba 14, 2000.

Akiwa na umri wa miaka 25 tu, mwanariadha huyu wa Uganda anajenga wasifu unaomfanya kuwa miongoni mwa wakimbiaji bora zaidi wa mbio ndefu katika kizazi chake.

Na mafanikio yake ya hivi karibuni yanaonesha kuwa ndio mwanzo mkoko waalika maua.

Mnamo Machi 2026, Kiplimo alitwaa tena rekodi ya dunia ya nusu-marathon kwa wanaume, akikimbia kilomita 21.1 kwa muda wa dakika 57 na sekunde 20 jijini Lisbon, Ureno. Alipunguza sekunde kumi kutoka kwenye rekodi iliyokuwepo awali.

Lakini mbio za barabarani ni sehemu moja tu ya safari yake.

Januari 2026, Kiplimo alishinda taji lake la tatu la dunia la mbio za nyika (cross-country) kwa wanaume, akithibitisha ubabe wake katika mchezo ambao kwa jadi umetawaliwa na Kenya na Ethiopia.

Pia amefanya mabadiliko ya kuvutia kuelekea kwenye mbio za marathon.

Baada ya kushika nafasi ya pili katika mbio zake za kwanza za marathon jijini London mwaka 2025, alishinda Marathon ya Chicago baadaye mwaka huo kwa muda wa saa mbili, dakika mbili na sekunde 23.

Kisha, mwezi Aprili 2026, alikimbia kwa muda wa saa mbili na sekunde 28 jijini London, na kuwa mmoja wa wakimbiaji wa marathon wenye kasi zaidi katika historia.

Safari yake ilianzia mashariki mwa Uganda, ambapo akiwa mtoto alikuwa akikimbia kilomita kadhaa kwenda na kurudi shule. Kwa kuwa alikulia katika familia ya wakulima, alihamasishwa na kaka zake wakubwa, ambao nao walikuwa wakimbiaji.

Leo hii, yeye ni mshindi wa medali ya shaba ya Olimpiki katika mbio za mita 10,000, bingwa wa dunia wa mbio za nyika (cross-country), na aliwahi kushikilia rekodi ya dunia ya nusu-marathon kwa wanaume.

Kwa Uganda, Kiplimo anawakilisha zaidi ya mafanikio ya mtu binafsi. Pamoja na nyota mwenzake Joshua Cheptegei, anasaidia kuifanya nchi hiyo kuwa nguvu kubwa duniani katika mbio za masafa marefu.

Na huku akiendelea kukimbiza rekodi za dunia swali moja linabaki: je, Jacob Kiplimo anaweza kufika mbali kiasi gani?

#