Inaripotiwa kuwa wahamiaji hao waliwasili katika mji mkuu wa Cameroon, Yaoundé, siku ya Jumatatu, wiki chache tu baada ya wahamiaji wengine tisa kupelekwa huko kimyakimya kufuatia sera ya Trump dhidi ya wahamiaji.

Rais Trump awafukuza raia wa Zimbabwe na Ghana kutoka Marekani hadi Cameroon

Ndege nyingine ya kuwafukuza wahamiaji kutoka Marekani imetua nchini Cameroon. Hata hivyo, waliorejeshwa si raia wa Cameroon na, kulingana na mawakili wao, hawana uhusiano wowote na nchi hiyo.

Kundi la hivi karibuni la wahamiaji linaripotiwa kuwasili Yaoundé siku ya Jumatatu, tarehe 16 Februari, wiki chache baada ya wahamiaji wengine tisa kupelekwa huko kimyakimya kufuatia sera yenye utata ya Trump ya kuwafukuza wahamiaji.

Ingawa utaifa wa wahamiaji wa hivi karibuni haukufahamika papo hapo, kundi la kwanza lilijumuisha wanawake watano na wanaume wanne kutoka nchi kama Zimbabwe, Morocco na Ghana, kulingana na ripoti za vyombo vya habari.

Mawakili wao, Alma David nchini Marekani na Joseph Awah Fru nchini Cameroon, waliiambia shirika la habari la The Associated Press kuwa kuwafukuza wahamiaji hao kwenda Cameroon kulikiuka maagizo ya mahakama za Marekani yaliyowapa ulinzi dhidi ya kufukuzwa.

Ikulu ya Marekani imethibitisha safari hiyo ya hivi karibuni ya ndege lakini haijatoa maelezo zaidi.

Mikataba ya siri

Cameroon si nchi pekee ya Afrika ambayo serikali ya Trump imepeleka wahamiaji kutoka nchi za dunia ya tatu. Katika miezi iliyopita, Marekani imewapeleka katika nchi za Sudan Kusini, Rwanda, Ghana, Uganda, Eswatini na Guinea ya Ikweta, kati ya waliorejeshwa wengine siyo wa kutoka nchi za Afrika.

Uhamisho huo, ambao ni sehemu ya msako mkali wa Trump dhidi ya wahamiaji, hufanywa chini ya mikataba yenye utata na mara nyingi ya siri, ambapo Marekani hulipa nchi zinazowapokea ili kuwahudumia wahamiaji ambao si raia wao.

Ripoti ya Kamati ya Mahusiano ya Kigeni ya Seneti ya Marekani inakadiria kuwa utawala wa Trump umetumia angalau dola milioni 40 kuwahamisha takriban wahamiaji 300 kwenda nchi zisizo zao.

Idara ya Mambo ya Nje ya Marekani pia ilisema kuwa Eswatini itapokea dola milioni 5.1 ili kupokea hadi wahamiaji 160 kutoka nchi za tatu.

Wahalifu waliotiwa hatiani Marekani

Mwaka jana, wanaume watano kutoka Vietnam, Jamaica, Cuba, Yemen na Laos, waliopatikana na hatia ya makosa makubwa nchini Marekani, walifukuzwa na kupelekwa Eswatini.

Ingawa nchi nyingi zinazowapokea wahamiaji hazijatoa maelezo ya kina, Ghana ilikanusha kupokea malipo kwa kuwahifadhi wahamiaji mwaka jana, ikisema hatua yake ilitokana na “roho ya Uanamajumui” (Pan-African spirit).

Marekani inadai kuwa inatekeleza sheria za uhamiaji, lakini wahamiaji waliorejeshwa na wanaharakati wanasema kuwa hatua hiyo ni ukiukaji wa haki za binadamu, kwa kuwa baadhi yao walikimbia nchi zao kutokana na hofu za usalama, na kufukuzwa kwao hakukufuata utaratibu unaostahili wa kisheria.

Raia wa nchi zinazowapokea pia wana hofu kuwa mara nyingi wahalifu sugu hujumuishwa miongoni mwa waliorejeshwa.

Comments

Comment

Comment Your email address will not be published. Required fields are marked*

No comments Yet

#