Kenya ni miongoni mwa timu nne za Afrika zilizofika hatua ya mtoano, ikiwa pamoja na Nigeria, Ghana, na wenyeji Morocco.
Timu ya wasichana ya Kenya, 'Junior Starlets', imeweka historia kwa kufika hatua ya 16 bora katika Kombe la Dunia la FIFA la Wanawake la U-17 kwa mara ya kwanza.
Junior Starlets walifuzu baada ya kupata ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Samoa katika mechi yao ya mwisho ya Kundi E siku ya Jumapili, Oktoba 25, katika Uwanja wa Mohammed VI mjini Salé, Morocco.
Mwanakombo Bakari alifunga mabao mawili, huku Brenda Awuor na Gaudancia Maloba nao wakifunga bao moja kila mmoja.
Kenya ilikuwa imepoteza mechi zake mbili za awali, ikifungwa 3-0 na China pamoja na 6-1 na Marekani.
Ushindi dhidi ya Samoa uliipandisha timu hiyo hadi nafasi ya tatu katika Kundi E, na kuifanya iwe miongoni mwa timu nne bora zilizoshika nafasi ya tatu ambazo zimefuzu kuingia hatua ya 16 bora.
Kwa upande mwingine, Japan ilimaliza kileleni mwa kundi lake ikiwa imeshinda mechi zote tatu, na itakuwa mtihani mkubwa kwa kikosi cha kocha Mildred Cheche watakapokabiliana katika mechi ya kuwania nafasi ya kuingia robo fainali.
Mechi hiyo imepangwa kufanyika Alhamisi, Oktoba 29, kuanzia saa 3 usiku kwa saa za Afrika Mashariki.
Kenya ni miongoni mwa timu nne za Afrika zilizofika hatua ya mtoano, ikiwa pamoja na Nigeria, Ghana, na wenyeji Morocco.
Zambia, mwakilishi wa tano kutoka Afrika, iliondolewa baada ya kupoteza mechi zote tatu za hatua ya makundi.

