Mswada huo umezua mjadala kuhusu uwazi na uwajibikaji katika mchakato wa uchaguzi, hasa ikizingatiwa kuwa Kenya inaelekea katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2027.

Bunge la Kenya lapitisha mswada wa kuondolewa sharti la kutangaza matokeo ya uchaguzi mubashara

Bunge la Kitaifa la Kenya limepitisha Mswada wa Marekebisho ya Sheria ya Uchaguzi Na. 2 wa mwaka 2024, unaopendekeza mabadiliko kadhaa katika mfumo wa uchaguzi nchini humo. Miongoni mwa mapendekezo hayo ni kuondoa sharti la kisheria linaloitaka Tume Huru ya Uchaguzi (IEBC) kutangaza matokeo ya uchaguzi mubashara katika vituo vya kupigia kura.

Hatua hiyo, iliyochukuliwa Alhamisi, Oktoba 22, imezua mjadala kuhusu uwazi na uwajibikaji katika mchakato wa uchaguzi, hasa ikizingatiwa kuwa Kenya inaelekea katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2027.

Kwa sasa, utangazaji wa matokeo mubashara huwawezesha wananchi, vyama vya kisiasa, wanahabari na waangalizi wa uchaguzi kufuatilia matokeo yanapotangazwa katika vituo vya kupigia kura. Pia, huwapa nafasi ya kulinganisha matokeo hayo na takwimu zinazowasilishwa baadaye katika vituo vya kujumlishia matokeo.

Mswada huo, uliwasilishwa na Kiongozi wa Wengi katika Bunge, Kimani Ichung’wah, pamoja na Kiongozi wa Wachache, Junet Mohamed. Unalenga kutekeleza mapendekezo yaliyotolewa na Kamati ya Kitaifa ya Mazungumzo (NADCO), huku ukipendekeza marekebisho ya baadhi ya vifungu vya Sheria ya Uchaguzi ya mwaka 2011.

Sehemu muhimu ya muswada huo ni Kifungu cha 22, kinachopendekeza marekebisho ya Kifungu cha 39 cha Sheria ya Uchaguzi. Kifungu hicho kinahusu namna matokeo ya uchaguzi yanavyobainishwa, kutumwa na kutangazwa.

Iwapo mapendekezo hayo yatakuwa sheria, IEBC haitakuwa tena na wajibu wa kisheria ulioainishwa wazi wa kuweka mfumo wa kurusha matangazo ya matokeo mubashara wakati yakitangazwa katika vituo vya kupigia kura.

Hata hivyo, mabadiliko hayo hayamaanishi kuwa tume hiyo itaacha kutuma au kuchapisha matokeo ya uchaguzi. IEBC itaendelea kuwa na jukumu la kuwasilisha matokeo kwa njia ya kielektroniki, kuthibitisha takwimu na kuweka fomu za matokeo za kila kituo cha kupigia kura kwenye tovuti inayopatikana kwa umma.

#