Miongoni mwa mapendekezo yaliyotangazwa na Rais ni kuondolewa kwa kodi ya mapato kwa wafanyakazi wanaopata shilingi 32,333 za Kenya au chini ya hapo kwa mwezi.

Kenya yaadhimisha ‘Siku ya Mashujaa’ huku Rais Ruto akiahidi nafuu ya kodi na ajira

Kenya inaadhimisha Siku ya Mashujaa, sikukuu ya kitaifa inayowenzi mashujaa wa nchi, huku Rais William Ruto akitangaza hatua mpya zinazolenga kupunguza shinikizo la kiuchumi kwa familia na kupanua fursa za ajira.

Akizungumza wakati wa sherehe za 63 za Siku ya Mashujaa mjini Eldoret, Ruto alikiri kuwepo kwa malalamiko ya umma kuhusu gharama kubwa ya maisha, kodi, na ukosefu wa ajira, hasa miongoni mwa vijana, akisema kuwa kushinda uchaguzi hakufuti wajibu wa serikali wa kuwajibika kwa raia.

Miongoni mwa mapendekezo yaliyotangazwa na Rais ni kuondolewa kwa kodi ya mapato (Pay As You Earn) kwa wafanyakazi wanaopata shilingi 32,333 za Kenya au chini ya hapo kwa mwezi.

Pia alielezea mipango ya kupunguza gharama za miamala ya ardhi, kupunguza ushuru wa uingizaji wa simu za mkononi, na kupanua fursa kwa vijana katika uchumi wa kidijitali.
Ruto alisema hatua hizo zinalenga kuwaacha Wakenya na pesa zaidi kwa ajili ya mahitaji muhimu, ikiwemo chakula, usafiri, na elimu, huku zikitengeneza fursa zaidi za kujipatia kipato.

Rais pia aliahidi kupanua mpango wa serikali wa mafunzo ya kazini (internship) na kuelezea ajenda pana ya kiuchumi inayolenga kuongeza uzalishaji wa kilimo, kuendeleza viwanda, na kukuza sekta ya huduma.

Hata hivyo, matangazo haya yanakuja huku kukiwa na wasiwasi unaoendelea kuhusu gharama ya maisha, wakati mamia ya watu walipoingia mitaani katika mji mkuu wa Nairobi na miji mingine kudai hatua za haraka kuchukuliwa kuhusiana na bei ya mafuta.

Siku ya Mashujaa huadhimishwa kila tarehe 20 Oktoba kwa ajili ya kuwaenzi wale waliochangia katika mapambano ya uhuru wa Kenya na maendeleo ya nchi hiyo baadaye.

Maadhimisho ya mwaka huu yameangazia upya fursa za kiuchumi na wajibu wa serikali kuleta maboresho yanayoonekana katika maisha ya wananchi.

Jumla ya Wakenya 264 wametambuliwa kama mashujaa wa taifa leo, akiwemo aliyekuwa Waziri Mkuu, marehemu Raila Odinga, ambaye ametunukiwa heshima hiyo baada ya kifo chake.

#