Mwaka 2013, Chivayo alianza kujiita “Sir Wicknell,” akijenga taswira ya utajiri na hadhi pale alipobadilika kutoka kuwa mtuhumiwa wa udanganyifu mpaka kuwa mkandarasi wa serikali mwenye mamilioni.
‘Amefeki’ kifo chake, baadhi wanaamini kwamba Wicknell Chivayo amefanya hivyo.
Lakini kama kweli amefariki, kuna swali moja ambalo kifo chake hakijajibu:
Chivayo alijengaje utajiri wake na kuanza kuitwa ‘Sir’ Wicknell?
Chivayo alizaliwa Zimbabwe tarehe 22 Novemba 1982.
Akiwa na miaka 15, aliacha shule baada ya familia yake kushindwa kulipa ada.
Mwaka 1998, akaanza kufanya kazi kama karani wa mishahara katika kampuni ya mabasi, ya Musanhi Transport.
Baadaye akaingia katika biashara ya simu, laini za simu na baadae biashara ya fedha za kigeni.
Mwaka 2004, maisha yake yakachukua mkondo mwingine.
Chivayo alihukumiwa kwa kumtapeli raia wa Afrika Kusini takriban dola 50,000, baada ya kumshawishi kuwa angeweza kuzidisha pesa zake na akafungwa miaka mitatu.
Alitoka gerezani mwaka 2006.
Baada ya kuachiliwa , mambo yakaanza kunoga zaidi.
Akaanza kujijenga upya.
Mwaka 2013, Chivayo alianza kujiita “Sir Wicknell,” akijenga taswira ya utajiri na hadhi pale alipobadilika kutoka kuwa mtuhumiwa wa udanganyifu mpaka kuwa mkandarasi wa serikali mwenye mamilioni.
Alianzisha Intratrek Zimbabwe, kampuni ya uhandisi na ujenzi wa miradi ya nishati na miundombinu, wakati mfumo wa umeme wa Zimbabwe ulipokuwa ukizorota.
Umiliki wa kampuni hiyo uliibua maswali. Uchunguzi wa The Zimbabwe Independent ulidai Chivayo alikuwa sura tu ya kampuni, iliyodaiwa kumilikiwa na Ibrahim Yusuf, raia wa Zambia aliyeishi Afrika Kusini, ambaye awali alihusishwa na biashara ya dawa za kulevya nchini Zambia huku kampuni hiyo ikiwa ilianzishwa mwaka 2001.
Mwaka wa 2014, Intratrek ilipewa mkataba wa Dola milioni 172.8 wa kujenga mradi wa umeme wa jua katika eneo la Gwanda nchini Zimbabwe.
Kampuni ikapokea takriban Dola milioni 5 malipo ya awali.
Lakini miaka minne baadaye, hakuna kilichokuwa kimejengwa.
Chivayo alikamatwa na kushtakiwa kuhusiana na matumizi ya fedha hizo.
Lakini mwaka 2019, Mahakama Kuu ikafuta mashtaka, ikasema mgogoro huo ulikuwa wa kimkataba, si wa jinai.
Na wakati huo huo, jina la Chivayo lilikuwa likizidi kukuwa.
Urafiki wake na Rais mpya aliyekuwa amechaguliwa mwaka 2017, Emmerson Mnangagwa, ulianza kushamiri.
Kisha akaanza kujipatia zabuni za vifaa vya uchaguzi katika nchi mbalimbali za Afrika ikiwemo Afrika kusini, Zambia na Namibia.
Lakini maswali kuhusu biashara zake hayakuisha.
Mwaka 2023, miamala kati ya kampuni zinazohusishwa naye na kampuni ya Afrika Kusini Ren-Form ilichunguzwa kuhusiana na mkataba wa vifaa vya uchaguzi nchini Zimbabwe.
Mamlaka za kupambana na rushwa zilisema hazikupata ushahidi wa udanganyifu wa manunuzi unaomhusisha Chivayo.
Kisha ikaja 2025.
Kampuni ya Afrika Kusini, TTM Global Medical Exports, ikatangazwa kushinda zabuni ya dawa na vifaa vya matibabu ya saratani nchini Zimbabwe yenye thamani ya Dola millioi 440.
Baadaye ilibainika kuwa Chivayo ndiye aliyekuwa mkurugenzi wa kampuni hiyo.
Lakini hata hivyo, maswali hayakuisha.
Aliendelea pia kuhusishwa na madai yasiyothibitishwa ya utakatishaji fedha, huku akidaiwa kupata asilimia kadhaa ya fedha hizo.
Na hapo ndipo “Sir Wicknell” akawa zaidi ya jina.
Magari ya kifahari. Zawadi za mamilioni kwa marafiki zake. Ndege binafsi. Na kuonekana akiwa karibu na viongozi wakubwa.
Kisha, Septemba 30, 2026, safari hiyo ya kifahari ikafikia mwisho, kwa ajali ya helikopta.
Wanaomfahamu kwa karibu wanasema kuwa alikuwa mnyenyekevu na aliyependa watu, lakini chanzo cha kila senti ya utajiri wake kitabaki kuwa fumbo ambalo jibu lake analo mwenyewe.
