Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi, aliwaelezea waandishi wa habari nje ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu pendekezo hilo, akisema kuwa Tehran pia itaanza upya mazungumzo yaliyokwama na Marekani kuhusu mpango wa nyuklia

Iran yapendekeza makubaliano na Marekani kufungua  Mlango-bahari wa Hormuz ndani ya siku saba

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi, amesema kuwa Tehran inaweza kufungua tena Mlango Bahari wa Hormuz ndani ya siku saba iwapo Marekani itakubali mpango uliowasilishwa kupitia Qatar.

Araghchi aliwaambia waandishi wa habari mjini New York, pembezoni mwa Mkutano wa 81 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, kuwa muda huo wa siku saba ungeanza mara tu Washington itakapokubali pendekezo hilo.

Alisema Marekani ingetarajiwa kuchukua hatua ndani ya siku nne au tano za kwanza, jambo ambalo lingeruhusu mlango huo kufunguliwa tena siku ya sita.

Mazungumzo kati ya Tehran na Washington kuhusu makubaliano ya mwisho yangeanza siku ya saba, alisema.

Waziri huyo wa mambo ya nje alisema hatua zilizotarajiwa kutoka kwa Washington tayari zilikuwa zimejumuishwa katika hati ya makubaliano iliyotiwa saini mjini Islamabad mwezi Juni.

"Iwapo kuna nia ya dhati kwa upande wa Marekani kufikia makubaliano na kufungua tena Mlango Bahari wa Hormuz, kila kitu kiko tayari sasa," alisema.

Araghchi alisema Iran imejitolea kuhakikisha usalama wa usafiri wa majini kupitia njio hiyo, lakini aliishutumu Washington kwa kukwamisha utekelezaji wa makubaliano hayo kupitia hatua za kijeshi zilizofuata.

Alisema Tehran bado iko tayari kwa diplomasia lakini inataka uhakikisho wa kuaminika dhidi ya mashambulizi mapya ya Marekani kabla ya kuanza duru nyingine ya mazungumzo.

Mazungumzo chanya na yenye tija

Ikulu ya Marekani ilisema maafisa wa Marekani wanafanya mazungumzo chanya na yenye tija na wapatanishi kuhusu suala la vita vya Iran.

Ikijibu maswali, ilisema Marekani inawezesha usafirishaji mkubwa wa mafuta kupitia Mlango wa Bahari wa Hormuz.

Pendekezo hilo, lililowasilishwa kwa Marekani na Qatar, linafanana na makubaliano ya muda yaliyofikiwa mwezi Juni, lakini likiwa na ratiba ya muda mfupi zaidi.

Katika ishara ya hivi karibuni ya hatua za kidiplomasia, Pezeshkian alikutana na Waziri Mkuu wa Qatar, Sheikh Mohammed bin Abdulrahman Al Thani, mapema siku ya Ijumaa.

Awali, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio, alisema, "Iwapo kutakuwa na fursa ya kubadilishana mawazo na ujumbe, tutafanya hivyo."

#