Sport
Vikosi vya serikali ya DRC vilianzisha mashambulizi dhidi ya kundi la waasi la M23 mashariki mwa nchi, kwa kutumia ndege zisizo na rubani kulenga eneo la kimkakati la uchimbaji madini lililokuwa likidhibitiwa na waasi hao.
Vyanzo vya usalama vililiambia shirika la habari la AFP siku ya Jumatano kwamba vikosi vya serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo vilifanya shambulio hilo kwa kutumia droni kulipiga eneo muhimu la mgodi uliokuwa umedhibitiwa na waasi mashariki mwa nchi.
Mapigano ya siku ya Jumatano yalijikita hasa katika maeneo yaliyo karibu na mji wa madini wa Rubaya, ambako waasi wa M23 walilengwa na shambulio la droni siku iliyotangulia, kwa mujibu wa vyanzo vya ndani na vya usalama vilivyozungumza na AFP.
Mgodi wa Rubaya huzalisha kati ya asilimia 15 hadi 30 ya uzalishaji wa dunia wa madini ya coltan, ambayo ni muhimu katika utengenezaji wa vifaa vya kielektroniki kama kompyuta na simu za mkononi.
Kundi la M23 limetwaa maeneo makubwa ya mashariki mwa DRC yenye utajiri wa rasilimali, na liliteka mgodi wa Rubaya katika jimbo la Kivu Kaskazini mwezi Aprili 2024.
Shambulio la M23 limelaaniwa kimataifa
Mwezi Disemba 2025, waasi wa M23 walizindua mashambulizi dhidi ya mji wa kimkakati wa Uvira katika jimbo la South Kivu karibu na mpaka wa Burundi.
Shambulio hilo lililaaniwa vikali kimataifa, ikiwemo kulaaniwa na Marekani, ambayo imekuwa mpatanishi katika makubaliano ya amani kati ya DRC na Rwanda.
Nchi ya Angola, ambayo pia nia mpatanishi, ilipendekeza usitishaji wa mapigano uanze tarehe 18 Februari, lakini mapigano bado yaliendelea.
Siku ya Jumatano, wapiganaji wa ndani wanaoungwa mkono na wanajeshi wa Congo walifanya mashambulizi katika maeneo kadhaa katika jimbo la Kivu Kaskazini, hasa katika eneo la Masisi kwa mujibu wa vyanzo vya ndani na vya usalama.
Serikali sanjari
Wapiganaji hao waliteka kijiji cha Kazinga siku ya Jumatano, takriban kilomita 20 kaskazini-magharibi mwa Rubaya, vyanzo hivyo vilisema.
Kwa mujibu wa wataalamu wa Umoja wa Mataifa, M23 imeanzisha serikali sanjari na serikali ya Congo ili kusimamia shughuli za mgodi wa Rubaya tangu ilipouteka.
“Mji wa kati wa Rubaya, watu wana hofu kubwa. Nilikwenda kuona eneo lilipopigwa na droni, lakini sikuruhusiwa kuingia,” mkazi mmoja aliambia AFP siku ya Jumanne, akiomba kutotajwa jina.
AFP haikuweza kuthibitisha idadi ya waliokufa kufuatia shambulio hilo, kwani mitandao ya simu katika eneo hilo imekatika tangu Jumanne.
Mapigano katika eneo la Kivu Kusini
Mapigano pia yaliripotiwa siku ya Jumatano katika nyanda za juu za Kivu Kusini, ambako jeshi la Congo linapambana na muungano wa wanamgambo wanaoshirikiana na M23.
Wataalamu wa masuala ya kikanda na vyanzo vya usalama waliiambia AFP kuwa jeshi la DRC limepata udhibiti wa kiasi wa anga yake kwa kutumia drones za masafa marefu kutoka China na Uturuki, pamoja na msaada wa wanajeshi wa kigeni.
Comments
No comments Yet
Comment