Waziri wa elimu ya juu anasema kuwa "wataondoa maneno ambayo yanawatambulisha kama watoto au wanyama, na kuongeza mafunzo yanayohimiza maadili yetu".
Serikali ya Burkina Faso inasema kuwa inabadilisha mtaala wake wa masomo ya historia, jiografia, na elimu ya siasa katika mwaka mpya wa masomo ili kuondoa "itikadi ya ukoloni" kwa wanafunzi.
"Tumeamua kuangalia upya mitaala yetu, kuondoa maneno ambayo yanatufanya sisi kuwa watoto au kama wanyama, na kuongeza mafunzo ya kuhimiza maadili yetu," Waziri wa Elimu ya Juu Moumouni Zoungrana alisema katika hafla moja ya serikali.
"Ukifungua vitabu vyetu, tunaonekana kama vitu visivyo na maana. Ushindi wetu haujaangaziwa; badala yake, wamaeangazia tulivyoshindwa na masuala yanayopotosha," Zoungrana alieleza.
Nchi hiyo ilikuwa koloni la Ufaransa hadi 1960.
Vitabu vya shule havijawahi kubadilishwa, kulingana na mwalimu mmoja wa historia na jiografia katika mji mkuu, Ouagadougou, lakini wizara imesambaza vipeperushi kueleza maneno gani yasitumiwe na masomo gani ya kuondolewa au kuongezwa.
"Hatutazungumzia waliosafiri na kuvumbua...lakini watakuwa wavamizi. Tutarekebisha mtazamo wa wapigania uhuru wa Afrika ambao walitajwa kuwa madhalimu au makatili katika vitabu vya zamani," mwalimu huyo alisema.
