Helikopta hiyo ilipata ajali siku ya Jumatano jioni eneo la Marondera, mashariki kwa mji wa Harare.
Polisi nchini Zimbabwe wamebadilisha idadi ya waliofariki katika ajali ya helikopta iliyosababisha kifo cha mfanyabiashara maarufu Wicknell Chivayo na mke wake, Lucy.
Polisi sasa wanasema ni watu watano pekee waliokuwa ndani ya helikopta, wakirekebisha ripoti ya awali ya watu sita. Watatu wengine ni msaidizi wa Lucy Chivayo, Senelisiwe Magagula, na marubani Kelvin T. Soda na Courage Mutavirwa.
Helikopta hiyo ilipata ajali siku ya Jumatano jioni eneo la Marondera, mashariki mwa mji wa Harare. Chanzo cha ajali hiyo bado kinachunguzwa.
Wakati huohuo Zimbabwe inasema uchunguzi kuhusu ajali hiyo umeanza na umma utafahamishwa kuhusu matokeo yake.
Ajali mbaya
Shirika la habari la taifa ZBC liliripoti kuwa watu hao walianza safari yao siku ya Jumatano kutoka eneo la Gandami, wilaya ya Chikomba ambako Chivayo alilelewa na yeye na mke wake walikuwa wanajenga nyumba huko.
Helikopta hiyo ilipata ajali dakika 40 baada ya kupaa kutoka shamba la Kudenga karibu la Marondera, mji ulioko karibu kilomita 70 kusini mashariki kwa Harare. Msemaji wa Serikali Nick Mangwana alisema kwenye mtandao X kuwa “hakukuwa na manusura”.
