Raia huyo wa Kenya alisafiri kupitia Uganda kabla ya kwenda kwa ndege hadi jijini Nairobi huku mamlaka zikifuatilia watu 28, ikiwemo jamaa zake na wahudumu wa afya.
Kenya imethibitisha mgonjwa wa kwanza wa Ebola baada ya raia wake aliyekuwa akiishi Jamhuri wa Kidemokrasia ya Congo kufariki alipowasili jijini Nairobi, Waziri wa Afya Aden Duale alisema siku ya Jumanne.
“Wizara ya Afya ingependa kuufahamisha umma kuwa imethibitisha mgonjwa wa kwanza wa Ebola ya aina ya Bundibugyo aliyesafiri kutoka nje ya nchi,” Duale alisema.
Mtu huyo alikuwa anaishi Congo katika kipindi cha miaka saba iliopita na aliugua mwezi mmoja kabla ya kurudi Kenya, kulingana na Wizara ya Afya. Alitibiwa katika hospitali mbalimbali DRC kabla ya kusafiri nchi jirani ya Uganda.
Baadaye alisafiri kwa ndege kutoka Uganda hadi Kenya akiwa ndani ya Jambojet iliokuwa na abiria 23 na kufika Katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta, jijini Nairobi siku ya Jumamosi Oktoba 3.
Mgonjwa huyo alipitia ukaguzi wa afya uwanja wa ndege kabla ya kuelekea kwenye dawati la uhamiaji, kulingana na wizara hiyo.
Jamaa na marafiki kisha wakampeleka kwenye Hospitali ya Nairobi, ambapo alilazwa akiwa sehemu ya peke yake.
Mgonjwa alibainika kuwa na Ebola aina ya Bundibugyo na baadaye alifariki dunia.
