Wachimba migodi 38 wafariki na wengine 27 kujeruhiwa baada ya mlipuko wa gesi katika mgodi wa Kampanin Zurak, jimbo la Plateau.

Mlipuko wa gesi mgodini Nigeria wauwa watu 38 Plateau

Wachimba migodi wasiopungua 38 wamefariki dunia kufuatia mlipuko wa gesi uliotokea Jumatano katika mgodi wa Kampanin Zurak, wilaya ya Bashar, jimbo la Plateau katikati mwa Nigeria, kwa mujibu wa vyanzo vya eneo hilo vilivyozungumza na AFP.

Tukio hilo pia limesababisha watu wengine 27 kujeruhiwa na kupelekwa hospitalini. Kaimu kiongozi wa jadi wa eneo hilo, Alhaji Aliyu Adamu Idris, alithibitisha vifo hivyo akisema idadi hiyo inaweza kuongezeka huku juhudi za uokoaji zikiendelea.

Shuhuda wa tukio, mchimba migodi Ibrahim Dattijo Sani, alisema mlipuko huo ulitokea asubuhi mapema wakati wachimba migodi walipokuwa bado chini ya ardhi. “Tulikuwa karibu na mgodi huo, watu walikuwa ndani ghafla tukasikia mlipuko mkubwa wa gesi,” alisema kwa njia ya simu.

Jimbo la Plateau linajulikana kwa shughuli za uchimbaji, huku mji mkuu Jos ukipewa jina la “Tin City” kutokana na historia yake ya madini ya bati. Hata hivyo, shughuli hizo zimepungua katika miaka ya hivi karibuni.

Nigeria imekumbwa mara kwa mara na ajali mbaya za migodini. Mwezi Septemba uliopita, watu wasiopungua 18 waliuawa katika jimbo la Zamfara baada ya mwamba kuporomoka katika mgodi haramu kufuatia mvua kubwa.

Chanzo: TRT Afrika

Comments

Comment

Comment Your email address will not be published. Required fields are marked*

No comments Yet

#