Afrika itawakilishwa na timu tano, zikiwemo wenyeji Morocco, pamoja na Nigeria, Ghana, Zambia na Kenya.

Kombe la Dunia toleo la 10 kwa wanawake U-17 kuanza nchini Morocco

Toleo la 10 la Kombe la Dunia la FIFA la Wanawake Chini ya Miaka 17 linaanza nchini Morocco siku ya Jumamosi, huku timu 24 kutoka mabara sita zikishindania taji hilo la dunia katika mji mkuu, Rabat.

Mechi nne zimepangwa kufanyika siku ya ufunguzi; Ujerumani itakabiliana na Argentina, huku mabingwa watetezi Korea Kaskazini wakikutana na wageni wa mara ya kwanza Puerto Rico, katika michezo ya awali itakayoanza saa 9:00 alasiri kwa saa za huko.

Wenyeji Morocco wataanza kampeni yao dhidi ya New Zealand saa 12:00 jioni, wakati Nigeria itapambana na Poland katika mchezo mwingine wa Kundi B kwa wakati huo huo.

Michuano hiyo inafanyika kuanzia tarehe 17 Oktoba hadi 7 Novemba—kipindi cha siku 22—huku mchezo wa fainali na ule wa kuwania nafasi ya tatu ukipangwa kufanyika siku ya kuhitimisha mashindano hayo.

Korea Kaskazini inaingia kwenye mashindano haya ikiwa ndiyo bingwa mtetezi, baada ya kushinda toleo la mwaka 2025 kwa kuifunga Uholanzi katika mchezo wa fainali.

Timu hiyo, ambayo imewahi kutwaa ubingwa mara nne, itakuwa inalenga kuongeza taji jingine kwenye rekodi yake na kudumisha ubabe wake katika soka la wanawake la vijana.

Afrika itawakilishwa na timu tano, zikiwemo wenyeji Morocco, pamoja na Nigeria, Ghana, Zambia na Kenya.

Morocco na Nigeria zitaanza kampeni zao siku ya Jumamosi, huku Ghana ikikabiliana na Norway na Zambia ikicheza dhidi ya Japan siku ya Jumapili. Kenya itaanza kampeni yake dhidi ya China siku ya Jumatatu.

Timu hizo 24 zimegawanywa katika makundi sita, kila moja likiwa na timu nne. Timu mbili za juu katika kila kundi, pamoja na timu nne zilizoshika nafasi ya tatu na kuwa na matokeo bora zaidi, zitafuzu kuingia hatua ya 16 bora.

Mashindano haya yanafanyika nchini Morocco kwa mwaka wa pili mfululizo, kufuatia uamuzi wa Baraza la FIFA kuipa nchi hiyo haki ya kuandaa mashindano haya yaliyopanuliwa na kupangwa kufanyika kila mwaka kwa kipindi cha kati ya mwaka 2025 na 2029.

#