Sport
Dollar
43,0024
0.08 %Euro
50,6408
-0.02 %Gram Gold
6.007,9200
0.7 %Quarter Gold
10.158,3200
0 %Silver
100,5000
1.57 %Tangu waasi wa M23 walipoanza tena mapigano mwaka 2021, wamechukua maeneo makubwa ya mashariki ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) yenye utajiri wa madini, hali iliyosababisha mgogoro mkubwa wa kibinadamu unaozidi kuongezeka.
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) imeshutumu Rwanda kwa kuua zaidi ya raia 1,500 katika mashariki mwa nchi hiyo tangu mapema Disemba, wakati waasi wa M23 walipoanzisha mashambulizi mapya.
Siku chache tu baada ya serikali za DRC na Rwanda kusaini makubaliano ya amani yaliyosimamiwa na Marekani tarehe 4 Disemba, waasi wa M23 waliuteka mji muhimu wa Uvira, jambo lililosababisha makumi ya maelfu ya watu kukimbilia nchi jirani ya Burundi.
DRC imeishutumu Rwanda kwa kuwaunga mkono waasi wa M23, tuhuma ambazo Rwanda imekanusha vikali.
Kwa mujibu wa taarifa ya DRC iliyotolewa Jumatano, “Idadi ya awali ya vifo vya raia waliouawa katika operesheni za Rwanda, iliyoanza tangu mwanzo wa Disemba zimehusisha matumizi ya mabomu na droni za ‘kamikaze’, imefikia zaidi ya watu 1,500.”
Ikiitaja hali hiyo kama “kitendo cha wazi cha uchokozi kutoka Rwanda,” DRC pia imeishutumu Rwanda kwa kutuma “vikosi vitatu vipya vya kijeshi vya Rwanda” katika jimbo la Kivu Kusini mashariki mwa nchi, kwa lengo la kusonga kuelekea “eneo la kimkakati la Kalemie” katika jimbo la madini la Tanganyika kusini-mashariki.
Ikiwa M23 watasonga kusini hadi Tanganyika, kundi hilo la waasi litapata ngome katika kaskazini-mashariki mwa eneo muhimu lililokuwa likijulikana awali kama jimbo la Katanga, ambalo ni kitovu cha uchimbaji madini nchini DRC.
Tangu walipochukua tena silaha mwaka 2021, waasi wa M23 wamechukua maeneo makubwa ya mashariki ya DRC yenye utajiri wa madini, na kuwalazimisha mamia ya maelfu ya watu kuhama makazi yao pamoja na kusababisha mgogoro mkubwa wa kibinadamu.
Baada ya kuanzisha mashambulizi yao ya hivi karibuni tarehe 2 Disemba, kufuatia kipindi cha miezi sita bila mapigano, kundi hilo liliteka Uvira tarehe 10 Disemba na hivyo kudhibiti mpaka wa nchi kavu kati ya DRC na mshirika wake Burundi.
Baada ya Washington kuituhumu Rwanda kwa kukiuka makubaliano ya amani, ambayo Rais wa Marekani Donald Trump aliyataja kuwa makubaliano ya “muujiza,” licha ya mashambulizi ya M23, kundi hilo lilitangaza tarehe 17 Disemba kwamba lingeondoka katika mji huo wenye maelfu ya wakazi.
Hata hivyo, Washington na DRC zimeonyesha mashaka kuhusu uhalisia wa tangazo hilo, huku vyanzo vya ndani vikiliambia shirika la habari la AFP siku yaAlhamisi kwamba wanachama wa M23 na maafisa wa polisi walibaki Uvira.
Mwanzoni mwa wiki, jeshi la DRC lilisema lilikuwa limerejesha udhibiti wa makazi kadhaa karibu na Uvira baada ya “mapigano makali.”
Kutekwa kwa mji huo kulikuja karibu mwaka mmoja baada ya M23 kuteka miji mikubwa ya mashariki ya Goma na Bukavu, ambayo ni miji mikuu ya majimbo ya Kivu Kaskazini na Kivu Kusini.
Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, zaidi ya watu 80,000 wamekimbilia Burundi kufuatia kusonga mbele kwa hivi karibuni kwa M23, huku angalau watu nusu milioni wakihamishwa makazi yao ndani ya jimbo la Kivu Kusini pekee.
Comments
No comments Yet
Comment