Dollar

0,0000

%

Euro

0,0000

%

Gram Gold

0,0000

%

Quarter Gold

0,0000

%

Silver

0,0000

%

Shirika la Umoja wa Afrika (AU) limetoa tahadhari baada ya serikali ya Marekani hivi karibuni kuagiza kusitishwa kwa ufadhili na kujihusiha katika baadhi ya mashirika ya Umoja wa Mataifa.

AU yatoa tahadhari baada ya Marekani kutangaza mpango wa kujiondoa kutoka kwa mashirika ya UN

Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika, Mahmoud Ali Youssouf, alisema Jumatatu kwamba ingawa Marekani ina haki ya kufanya maamuzi kuhusu masuala yake ya kimataifa, hatua ya hivi karibuni ya Washington inaweza kuwa na athari kubwa barani Afrika.

Kiongozi huyo wa AU alisisitiza maelezo ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, kuhusu umuhimu wa mfumo imara, unaofaa, na unaojumuisha washirika wengi.

Kwa mujibu wa Youssouf, dunia kwa sasa inakabiliwa na migogoro kadhaa, ikiwemo mizozo ya silaha, athari za mabadiliko ya tabianchi, hali ngumu ya kiuchumi, na tishio la afya ya umma. Kiongozi wa AU alisema katika taarifa yake kwamba mpango maalum wa ufadhili una jukumu muhimu katika kupunguza changamoto hizi.

Matumaini kwenye mazungumzo

Kulingana na Umoja wa Afrika, baadhi ya mashirika ya Umoja wa Mataifa yaliyoathirika na uamuzi wa Marekani yana nafasi muhimu katika kusaidia maendeleo na jitihada za amani barani Afrika.

Haya ni pamoja na Kamisheni ya Uchumi ya Umoja wa Mataifa kwa Afrika (ECA), Idara ya Masuala ya Kiuchumi na Kijamii (DESA), Jukwaa la Umoja wa Mataifa wa Biashara na Maendeleo (UNCTAD), Ofisi ya Mshauri Maalum wa Afrika, UN Women, Bodi ya Mfuko wa Umoja wa Mataifa wa Idadi ya Watu (UNFPA), Kamisheni ya Ujenzi wa Amani na Mfuko wa Ujenzi wa Amani, pamoja na mifumo iliyoundwa kulinda watoto katika migogoro ya silaha.

AU imetahadharisha kwamba kupunguzwa kwa ufadhili kwa mashirika haya kunaweza kuathiri mafanikio ya maendeleo, jitihada za kuimarisha amani, na uimara wa jamii, hasa katika nchi zilizo hatarini au zinazokabiliwa na migogoro.

Tume ya Umoja wa Afrika inatumai kwamba mazungumzo yanayoendelea kati ya Marekani, Umoja wa Mataifa, na washirika wengine wa kimataifa yataweza kusaidia kubaini njia za kudumisha kazi muhimu za kimataifa.

Mnamo Januari 7, serikali ya Rais Donald Trump ilitangaza kwamba Marekani hivi karibuni itajiondoa katika mashirika 31 ya Umoja wa Mataifa na mashirika 35 yasiyo ya Umoja wa Mataifa, ikirejelea haja ya kupunguza matumizi ya serikali.

Comments

Comment

Comment Your email address will not be published. Required fields are marked*

No comments Yet

#