Mkutano huo katika Kambi ya Kijeshi ya Ovda unajiri wakati kukiwa na uwezekano wa mazungumzo kuhusu kuanza tena mashambulizi dhidi ya Iran.

Waziri wa Ulinzi wa Marekani Pete Hegseth akutana na Netanyahu katika ziara ya kushtukiza Israel

Waziri wa Ulinzi wa Marekani Pete Hegseth amekutana na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu wakati wa ziara ya kushtukiza nchini Israel, huku kukiwa na majadiliano kati ya Marekani na Israel kuhusu uwezekano wa kuanzisha tena mashambulizi dhidi ya Iran, Axios imeripoti, ikitaja vyanzo viwili vinavyofahamu kuhusu mkutano huo.

Mkutano huo ulifanyika katika kambi ya kijeshi ya Ovda kusini mwa Israel, ambapo ndege za kivita za Marekani huenda kuwekewa mafuta, kulingana na ripoti.

Hegseth aliweka picha na ujumbe kwenye mitandao ya kijamii wakati wa ziara yake kwa majeshi ya Marekani, yenye majukumu ya oparesheni za Mashariki ya Kati.

"Kama kawaida, imekuwa heshima kwa wanajeshi wetu wa CENTCOM leo. Wanajeshi bora wa nchi yetu, walio katika oparesheni ya kihistoria," alisema.

Ziara hii inajiri siku nane kabla uchaguzi wa wabunge wa Israel Oktoba 27.

Wizara ya Ulinzi na Ubalozi wa Israel haujazungumzia suala hilo, ilhali ofisi ya Netanyahu pia haikujibu kuhusu ombi la kuzungumzia hilo.

Uungwaji mkono katika uchaguzi

Ziara hii inafuata hatua ya Rais wa Marekani Donald Trump kumuunga mkono Netanyahu siku ya Jumapili wakati wakielekea kwenye uchaguzi.

Katika ujumbe mrefu kwenye mtandao wake wa kijami wa Truth Social, Trump alisema kuwa "Anamuunga mkono kikamilifu" katika mipango ya kiongozi wa Israel kutaka kuchaguliwa tena.

Trump alipongeza uongozi wa Netanyahu na ushirikiano wake na Marekani, hasa katika kukabiliana na Iran.

Pia alionya kuwa Marekani huenda ikalazimka kuchukua jukumu hilo peke yake iwapo wapiga kura wa Israel watamchagua kiongozi mwingine.

#