Fedha hizo zinadaiwa zilikuwa ndani ya makochi katika shamba la rais.
Mahakama nchini Afrika Kusini imewapata na hatia washukiwa wawili kati ya watatu wanaodaiwa kuiba Dola 580,000 kutoka kwa shamba la Rais Cyril Ramaphosa la Phala Phala mkoa wa Limpopo mwaka 2020.
Mahakama ya Modimolle iliwapata Imanuwela David na Floriana Joseph na hatia ya kuhusika katika wizi, huku mshukiwa wa tatu, Ndilinasho Joseph, akiachiwa huru.
Hakimu Peter Manthata alisema taarifa za simu zilitoa ushahidi wa kutosha wa kumhusisha David na Floriana na wizi huo, ambao ulihusisha wizi wa fedha zilizokuwa ndani ya makochi kwenye shamba la rais.
“Kwa kuzingatia ushahidi kwa ujumla, jambo peke linalojitokeza ni mawasiliano kati ya mshukiwa wa kwanza na wa pili kuhusu Dola zilizokuwa zimefichwa chini ya kochi kwenye nyumba ya shamba la Phala Phala. Kwa hiyo, nimejiridhisha kuwa wawili hao walipanga njama ya kuvunja nyumba na kuiba pesa zilizosemekana kuwemo ndani humo.”
Mahakama pia iliambiwa kuwa David alitumia sehemu ya fedha alizoiba kumnunulia aliyekuwa mpenzi wake wakati huo gari na nyumba, shirika la habari la taifa SABC liliripoti.
TRT Afrika Swahili — TRT Afrika Swahili
