Sport
Dollar
42,0187
0.15 %Euro
49,0800
-0.27 %Gram Gold
5.725,2700
-1.68 %Quarter Gold
10.114,3100
1.99 %Silver
70,0500
-4 %Uturuki ni mshirika wa kuaminika, anayejenga, kuwekeza, kusikiliza na kuchukua hatua sambamba na matarajio ya Afrika, alisema Kamishna wa Maendeleo ya Kiuchumi wa Umoja wa Afrika, Francisca Tatchouop Belobe.
Jukwaa la 5 la Biashara na Uchumi kati ya Uturuki na Afrika (TABEF) limehitimishwa Ijumaa mjini Istanbul, likidumisha moja ya ushirikiano unaokua kwa kasi zaidi kati ya nchi za Kusini mwa dunia.
Kwa kauli mbiu ya: “Kuhamasisha Mahusiano ya Uturuki na Afrika kwa Manufaa ya Pande Zote”, jukwaa hili lilikutanisha zaidi ya washiriki 4,000 wakiwemo wakuu wa nchi, mawaziri, mabalozi na viongozi wa sekta binafsi kutoka barani Afrika na Uturuki.
Katika hotuba yake kuu iliyosubiriwa kwa hamu, Kamishna Belobe alieleza kuwa ushirikiano wa Uturuki na Afrika “siyo tu halisi, bali hauwezi kurudishwa nyuma.”
Kauli hiyo inaonyesha makubaliano yanayokua miongoni mwa viongozi kuwa ushirikiano huu hauko tena katika hatua ya kuanza, bali tayari umejengeka na unabadilisha namna nchi zinazoenedela kiuchumi zinavyofanya biashara.
“Mshirika wa kuaminika”
“Uturuki siyo mgeni anayepita,” alisema Kamishna Belobe. “Ni mshirika wa kuaminika – anayejenga, kuwekeza, kusikiliza, na kuchukua hatua sambamba na matarajio ya Afrika.”
Kamishna huyo alionyesha ukuaji mkubwa wa kiuchumi kati ya pande hizi mbili:
“Katika kipindi kisichozidi miongo miwili, biashara kati ya Afrika na Uturuki imeongezeka kutoka dola bilioni 4.5 za Marekani mwaka 2003 hadi zaidi ya dola bilioni 40.7 mwaka 2024.”
Ukuaji huu umelifanya Uturuki kuwa miongoni mwa washirika watano wa juu wa kibiashara wasiokuwa wa Kiafrika barani humo. Kwa lengo la pamoja la kufikia dola bilioni 50 ifikapo 2026, Belobe alisema kasi ya maendeleo sio tu inaendelea – bali inazidi kuongezeka.
“Tunaona uhusiano unaoongozwa na dhamira ya kisiasa na matarajio ya sekta binafsi,” alisema. “TABEF ni ushahidi kuwa huu siyo diplomasia tu – huu ni utekelezaji.”
Ushirikiano wa zaidi ya biashara
Uwekezaji wa moja kwa moja wa Uturuki barani Afrika (FDI) sasa umepita dola bilioni 8.5, ukisaidia miradi katika nishati mbadala, miundombinu ya kidijitali, viwanda, na sekta nyingine.
Zaidi ya kampuni 1,500 za Kituruki zinafanya kazi Afrika, nyingi zikiwa na ushirikiano wa moja kwa moja na biashara ndogo na za kati (SMEs) za Kiafrika na taasisi za ndani.
“Uturuki haiwekezi ili kuchota rasilimali, bali kwa ajili ya mabadiliko,” alisisitiza Belobe. “Inasaidia biashara zetu ndogo, inashirikisha teknolojia, inajenga uwezo na inaimarisha minyororo ya thamani – huu ni mpango wa muda mrefu unaotekelezwa.”
Katika eneo la maonyesho ya jukwaa hilo, Belobe alikutana na wajasiriamali na wavumbuzi kutoka pande zote za bara.
Alieleza mfano wa kampuni ndogo ya Kiafrika inayotumia akili mnemba kubadilisha sekta ya usafirishaji, na kampuni ya Kituruki inayoshirikiana kuunda suluhisho la nishati endelevu vijijini.
“Hizi si hadithi za kusisimua tu – ni ushahidi,” alisema. “Hivi ndivyo ushirikiano wa karne ya 21 unavyopaswa kuwa – ubunifu wa pamoja, uvumbuzi na manufaa ya pande zote.”
Alisisitiza ya kwamba Afrika siyo tu wazi kwa biashara – bali inaunda mustakabali wa biashara.
Mwaka 2024, Afrika ilivutia uwekezaji wa moja kwa moja wa dola bilioni 97, ikiwa ni ongezeko la asilimia 7.5 kutoka mwaka uliopita.
Biashara ya ndani ya bara (intra-African trade) ilifikia dola bilioni 280, huku nchi 15 zikiripoti ukuaji wa Pato la Taifa (GDP) wa zaidi ya 5%, licha ya changamoto za kiuchumi duniani.
Faida ya idadi kubwa ya watu Afrika
Afrika ina faida kubwa ya idadi ya watu, ikiwa na wastani wa umri ni miaka 19.5, na inatarajiwa kufikia watu bilioni 2.5 ifikapo 2050 – ikifanya kuwa na hifadhi kubwa zaidi ya vipaji na nguvu kazi duniani.
“Ifikapo 2030, asilimia 43 ya vijana wote duniani watakuwa waafrika,” alisema Belobe. “Sisi ni bara changa zaidi – na hiyo changamoto, hiyo nishati, ndiyo mustakabali.”
Mpango wa Eneo Huru la Biashara Barani Afrika (AfCFTA), ni msingi wa mabadiliko ya kiuchumi ya bara chini ya Ajenda 2063 ya AU.
Ikiwa na thamani inayokadiriwa kufikia dola trilioni 6.7 kufikia 2035, AfCFTA inatarajiwa kuwa soko kubwa zaidi duniani la biashara huru.
Belobe alisifu msaada wa Uturuki kwa ajenda hii ya bara, akisema Ankara haijajikita tu katika mikataba ya pande mbili, bali pia inaunga mkono muunganiko wa kikanda.
“Uturuki inaelewa kuwa nguvu ya Afrika iko katika umoja wake; katika kujenga minyororo ya thamani ya kikanda, miundombinu ya kuvuka mipaka, na sheria za biashara zilizoratibiwa,” alisema.
Jukwaa la TABEF, lililofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Istanbul, lilikuwa zaidi ya hafla ya kidiplomasia – lilikuwa ni jukwaa la kazi, ambapo mikataba ilijadiliwa, ushirikiano ulitangazwa, na maeneo ya uwekezaji ya baadaye yalibainishwa.
Mada mbalimbali zilijadiliwa, kutoka nishati ya kijani hadi miundombinu ya kidijitali, huku Uturuki ikisisitizwa kuwa mwekezaji mwaminifu na anayeitikia haraka.
“Tumeona zaidi ya hotuba – tumeona suluhisho,” Belobe alisema katika kikao cha mwisho. “Jukwaa hili linaweza kumalizika leo, lakini safari yetu inaendelea. Ushirikiano kati ya Uturuki na Afrika si tu uko hai – unakua, unachanuka, na wa kuendelea.”
Ushirikiano huu ulisifiwa kuwa mfano wa diplomasia ya kiuchumi inayotegemea maslahi ya pamoja, heshima ya pande zote, na uwezo wa mabadiliko ya kweli.
Comments
No comments Yet
Comment