Uamuzi huo unakuja wakati mashambulizi ya wapiganaji wa kundi la Houthi yakiongezeka, huku Uingereza ikiimarisha msaada wake wa kijeshi wa kujihami kwa Saudi Arabia kufuatia mashambulizi mapya.

Uingereza kupeleka ndege za kivita Saudi Arabia kuilinda dhidi ya mashambulizi ya Wahouthi

Serikali ya Uingereza imetangaza kuwa itapeleka ndege za kivita aina ya Typhoon (RAF) kutekeleza operesheni za kujihami, kwa lengo la kusaidia kuilinda Saudi Arabia dhidi ya mashambulizi yanayoongezeka ya wapiganaji wa kundi la Houthi.

Ndege hizo zitafanya operesheni za kujihami dhidi ya mashambulizi ya anga ili kulinda miji ya Saudi Arabia pamoja na miundombinu yake muhimu dhidi ya mashambulizi ya anga, Wizara ya Ulinzi ya Uingereza imesema katika taarifa siku ya Jumanne.

Aidha, kwa mujibu wa shirika la habari la Bloomberg, iliyonukuu maafisa wa Uingereza wanaofahamu suala hilo, Uingereza pia itatoa ndege ya usafirishaji wa kijeshi aina ya Atlas A400M pamoja na washauri wa kijeshi.

Mwezi Septemba, Uingereza ilitangaza msaada wa ziada wa kijeshi kwa Saudi Arabia kufuatia kuanza tena kwa mashambulizi ya wapiganaji wa Houthi. Msaada huo ulijumuisha ndege ya RAF aina ya Voyager, inayotumika kuweka mafuta kwa ndege nyingine zikiwa angani. Hata hivyo, tangazo hilo halikujumuisha msaada wa ndege za kivita.

Mashambulizi ya wapiganaji wa Houthi yameongezeka katika wiki za hivi karibuni.

Mamlaka za Yemen zilisema Jumanne kuwa shambulio lililolenga kambi ya mafunzo ya kijeshi kwa vikosi serikali siku ya Jumatatu liliua watu 60. Kwa mujibu wa mamlaka hizo, hilo ndilo shambulio lililosababisha vifo vingi zaidi tangu mapigano nchini humo yalipoanza kuongezeka kwa kasi miezi mitatu iliyopita.

#