Matamshi ya Rais wa Marekani yanajiri wakati gazeti la The New York Times likiandika kuwa majeshi ya Marekani na Israel yameandaa mpango wa kufanya mashambulizi mengine baada ya uchaguzi wa Marekani wa nusu muhula.

Trump asema Marekani haijadiliani na Iran, aashiria kuwashughulikia 'hivi karibuni'

Rais wa Marekani Donald Trump anasema kuwa taifa lake halifanyi majadiliano na Iran, akiongeza kuwa “kuna jambo litafanyika hivi karibuni.”

“Hapana, hatujadiliani,” Trump aliwaambia waandishi wa habari aliporudi kutoka mkutano wa siasa jimbo la Carolina Kusini siku ya Jumatano. “Tutalishughulikia hilo hivi karibuni.”

“Watu wengi wanadhani itakuwa baada ya uchaguzi, na tutaona kile kitakachotokea,” aliongeza.

Awali katika mkutano huo, Trump alisema Marekani inaweza kumaliza vita vyake na Iran lakini inahitaji kuhakikisha kuwa kuna suluhu ya kudumu.

“Vitamalizika hivi karibuni. Tunaweza kuachana navyo sasa, lakini tunataka kuhakikisha kuwa kuna suluhu ya muda mrefu,” alisema.

Alidai kuwa Marekani imeishinda Iran kijeshi na kiuchumi, akiongeza Iran “haiwezi tena kuwa na silaha za nyuklia.”

Matamshi yake yanajiri baada ya gazeti la The New York Times kuripoti kuwa majeshi ya Marekani na Israel yameandaa mpango wa kuanzisha tena mashambulizi dhidi ya Iran baada ya kumalizika kwa uchaguzi wa nusu muhula, wakinukuu maafisa wa Marekani na wengine ambao wanafahamu kuhusu maamuzi hayo.

Ripoti hiyo inaashiria wazi kuwa Trump ataidhinisha mashambulizi hayo, ikieleza kuwa mara kadhaa amefanya maamuzi tofauti na ushauri aliopewa ya kufanya mashambulizi mwaka huu.

Afisa mmoja wa Ikulu ya Marekani ameiambia Times kuwa serikali haizungumzii mipango ya kijeshi “ambayo ipo au pengine haipo.”

Marekani na Israel ilianzisha vita dhidi ya Iran Februari 28, kusababisha Iran kujibu kwa mashambulizi ya makombora na droni katika kanda pamoja na kufunga Mlango Bahari wa Hormuz, njia muhimu inayotumika kufikisha nishati.

Makubaliano yaliyotiwa saini mwezi Juni na Marekani na Iran kufuatia upatanishi wa Pakistan na Qatar yamekwama huku kukiwa na kutofautiana, ikiwemo kuhusu utumiaji wa Mlango Bahari huo.

#