Tukio hilo limetokea wakati mashambulizi ya makombora na ndege zisizo na rubani yanayofanywa na wapiganahi wa Houthi dhidi ya Saudi Arabia yakiongezeka.

Saudi Arabia yazuia kombora katika anga ya mji wa Madinah

Muungano unaoongozwa na Saudi Arabia umetangaza kuzuia na kuharibu kombora la 'cruise' katika eneo la Madina, magharibi mwa Saudi Arabia.

Msemaji wa muungano huo, Meja Jenerali Turki al-Maliki, alitangaza tukio hilo kupitia taarifa fupi kwenye mtandao wa kijamii wa X siku ya Alhamisi.

Taarifa hiyo haikubainisha aliyelirusha kombora hilo wala shabaha iliyokuwa ikilenga. Pia, haikutoa maelezo kuhusu vifo, majeruhi au uharibifu.

Tukio hilo limetokea wakati mashambulizi ya makombora na ndege zisizo na rubani yanayofanywa na wapiganahi wa Houthi dhidi ya Saudi Arabia yakiongezeka.

Muungano huo umewalaumu Wahouthi kwa shambulizi la ndege isiyo na rubani dhidi ya kituo cha usambazaji wa umeme cha Taibah, katika eneo la Madina, Septemba 29

Kwa mujibu wa al-Maliki, shambulizi hilo liliharibu transfoma, lakini halikuharibu mfumo wa gridi ya umeme.

Kituo hicho husambaza umeme katika Msikiti wa Mtume, mojawapo ya maeneo matakatifu zaidi katika Uislamu.

Tukio la Alhamisi lilitokea saa chache baada ya muungano huo kutangaza mapema siku hiyo kuwa ulikuwa umedungua na kuharibu ndege isiyo na rubani katika Mkoa wa Mashariki wa Saudi Arabia.

Siku moja kabla, muungano huo ulitangaza kuwa ulikuwa umeliharibu kombora la balistiki lililorushwa na kundi la Wahouthi kutoka Yemen kuelekea Riyadh, mji mkuu wa Saudi Arabia.

Saudi Arabia imekuwa ikiongoza muungano wa kijeshi unaounga mkono serikali ya Yemen dhidi ya wapiganaji wa Houthi tangu mwaka 2015. Kundi hilo limekuwa likidhibiti mji mkuu, Sanaa, na majimbo kadhaa ya Yemen tangu mwaka 2014.

#