Matokeo ya awali ya uchaguzi nchini Israel yanaonyesha chama cha Likud kinachoongozwa na Benjamin Netanyahu kikiongoza. Mpinzani wake wa chama cha Yashar cha Gadi Eisenkot akishika nafasi ya pili.
Chama cha Likud kinachoongozwa na Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, kinaongoza hadi sasa katika uchaguzi wa wabunge.
Chama hicho kimepata zaidi ya asilimia 24 ya kura zilizohesabiwa. Chama cha Yashar, kinachoongozwa na Gadi Eisenkot, aliyewahi kuwa mkuu wa majeshi ya Israel, kimefuatia kwa asilimia 16, kwa mujibu wa gazeti la Israel la Yedioth Ahronoth.
Kwa mujibu wa taarifa za vyombo vya habari, Kamati Kuu ya Uchaguzi ilikuwa imehesabu asilimia 30 ya kura zote zilizopigwa.
Muungano wa Together, unaoongozwa na aliyewahi kuwa waziri mkuu wa Israel, Naftali Bennett, umeshika nafasi ya tatu kwa kupata asilimia 8.8 ya kura. Joint List imepata asilimia 5.9, huku chama cha Warabu (Ra’am) kikipata asilimia 2.75.
Makadirio ya kura za maoni na idadi ya waliojitokeza kupiga kura
Matokeo hayo ya awali yanakuja baada ya makadirio ya kura yaliyotolewa na vituo vikuu vya televisheni kubadilika mara kadhaa.
Hapo awali, makadirio yaliyorekebishwa ya Kituo cha Televisheni cha Channel 12 yalionyesha kuwa kambi ya mrengo wa kulia inayomuunga mkono Netanyahu ingeweza kupata viti 52, huku muungano wa upinzani unaoongozwa na Eisenkot ukitarajiwa kupata viti 49. Vyama vya Waarabu vilikadiriwa kupata viti 19.
Hata hivyo, makadirio yaliyosasishwa na Shirika la Utangazaji la Umma la Israel pamoja na Channel 13 yalionyesha kuwa kambi hizo mbili kuu zingepata viti 51 kila moja, huku vyama vya Waarabu vikikadiriwa kupata viti 18.
Kwa mujibu wa makadirio yote hayo, hakuna kambi iliyotarajiwa kufikisha viti 61 vinavyohitajika ili kupata wingi wa wabunge katika bunge lenye viti 120 na hivyo kuwa katika nafasi ya kuunda serikali yenye uungwaji mkono wa wengi.
Wakati huohuo, idadi ya wapiga kura nchini Israel ilifikia asilimia 77.7. Kwa mujibu wa takwimu zilizothibitishwa na Kamati Kuu ya Uchaguzi, kiwango hicho ni cha juu zaidi kurekodiwa katika uchaguzi wa kitaifa nchini humo tangu mwaka 1999.

