Kituo cha Kudhibiti Magonjwa barani Afrika (Africa CDC) kimeona kuwepo kwa 'hatari kubwa' huku maambukizi yakienea katika kanda tatu, na majaribio ya chanjo yakitarajiwa kuanza mwishoni mwa mwezi Oktoba.
Nigeria imethibitisha maambukizi ya kwanza ya ugonjwa wa Ebola katika mlipuko wa sasa, huku Kenya ikiwa na maambukizi yake ya tisa, kuzua hofu kuhusu kusambaa kwa ugonjwa huo barani Afrika.
Mgonjwa wa Nigeria ni mwanamke ambaye alisafiri kutoka Uganda hadi mji mkuu wa nchi hiyo, Abuja, na alibainika baada ya kutibiwa katika hospitali binafsi kwa siku kadhaa, Waziri wa Afya Muhammad Ali Pate alisema siku ya Jumanne. Amewekwa kando na anatibiwa, huku mamlaka zikiwa zinawafuatilia watu 44 waliotangamana naye.
Maambukizi ya sasa ya Kenya ni mvulana wa miaka 24 ambaye alibainika baada ya kuwa karantini alipoonekana na dalili. Ni jamaa wa karibu wa mgonjwa wa kwanza aliyethibitishwa, ambaye alifariki Nairobi Oktoba 5, Wizara ya Afya ilisema.
Kenya ina maambukizi tisa, ikiwemo mtu mmoja kufariki. Mamlaka zinasema kuwa maambukizi yote yako kwenye kundi moja, huku ikiwa hakuna ushahidi wa maambukizi zaidi ya kundi hilo. Wamewafuatilia na kuwaweka karantini watu 134 kati 135 waliotambuliwa kutangamana na kusema kuwa wagonjwa waliopo wanaendelea vizuri na matibabu.
Mlipuko huko, uliosababishwa na virusi vya Bundibugyo, sasa umeathiri nchi nne — DRC, Uganda, Kenya na Nigeria — na kufikia sasa watu karibu 9,400 wameambukizwa na wasiopungua 4,500 kufariki, kulingana na takwimu katika taarifa kadhaa.
‘Mlipuko umesambaa maeneo kadhaa’
Jean Kaseya, mkurugenzi mkuu wa Africa CDC, ameonya kuwa mlipuko huu wa Ebola umesambaa na kuathiri kanda tatu za Afrika.
“Huku asilimia 50 ya watu wanaoambukizwa wakifariki nchini DRC, tunakabiliwa na hatari kubwa,” Kaseya alisema kwenye mtandao wa kijamii wa X, akitoa wito kwa jamii ya kimataifa kusaidia kwa fedha, dawa na wahudumu wa afya.
Hakuna chanjo iliyoidhinishwa au dawa kwa virusi vya sasa, na Shirika la Afya Duniani (WHO) limeonya kuwa mlipuko huo unazidi uwezo wa juhudi za kukabiliana na ugonjwa huo.
Uwezekano wa majaribio ya kwanza ya chanjo yanatarajiwa kufanyika mwishoni mwa mwezi Oktoba, kulingana na WHO.

