Mgogoro kati ya binadamu na wanyamapori unasababishwa kwa kiasi kikubwa na ushindani wa ardhi, chakula na maji kati ya wanadamu na wanyama.

Migogoro ya wanyamapori na binadamu


Usalama wa wanyamapori sasa ni jambo linalotia wasiwasi hasa katika mbuga za wanyama Afrika Mashariki.

Simba 10 wamekutwa wamekufa katika eneo la Ndutu katika  Hifadhi la Ngorongoro nchini Tanzania, na kuzua wasiwasi kwamba huenda wanyama hao walipewa sumu ya sianidi ambayo hutumiwa katika kilimo hasa kwa ajili ya kudhibiti wanyama-mwitu wanaowinda wadudu.

Vifo hivyo ni hasara kubwa kwa Tanzania ambayo ina sifa ya kuwa na idadi kubwa ya simba duniani.

Sensa ya kitaifa ya wanyamapori iliyotolewa mwaka huu inakadiria kwamba nchi hiyo ina takriban simba 17,200.

Tukio jengine la kushtusha ni katika nchi jirani ya Kenya, ambapo tembo 18 walipatikana wamekufa katika Hifadhi ya Taifa ya Amboseli.

Vipimo vya awali vya maabara  pia viligundua sianidi katika sampuli sita kati ya kumi zilizochunguzwa.

Wataalamu wanasema vifo hivyo ni ishara kwamba mgogoro kati ya binadamu na wanyamapori lazima ushughulikiwe.

Chanzo ni nini?

Mgogoro kati ya binadamu na wanyamapori unasababishwa kwa kiasi kikubwa na ushindani wa ardhi, chakula na maji kati ya wanadamu na wanyama.

Wataalamu wa wanyama pori wanasema kwamba kuongezeka kwa idadi ya watu kumesababisha uvamizi katika maeneo ambayo kiasili yanakaliwa na wanyama.

Kwa hivyo, shughuli za binadamu ikiwemo ukulima na makazi zinazidi kusababisha migogoro katika maeneo ya wanyama pori.

Hii inawaleta wanyama karibu na watu. Tembo wanaweza kuvamia mazao, huku simba na wanyama wengine wanaowinda mifugo wanaweza kushambulia mifugo, wakati mwingine na kusababisha mauaji ya kulipiza kisasi.

Ukame unaweza kufanya tatizo kuwa baya zaidi huku watu na wanyamapori wakishindania vyanzo vya maji vinavyozidi kuwa vichache.

Katika baadhi ya maeneo, mizoga ya mifugo huekwa dawa za kuua wadudu za kilimo au vitu vingine vyenye sumu ili kuua wanyama wanaowinda kama vile simba na fisi wanaoshambulia mifugo.

Kwa hivyo, migogoro kati ya binadamu na wanyamapori inakupunguzwaje?

Hakuna suluhisho la moja kwa moja.

Kulinda mashamba na mifugo kwa kutumia vizuizi imara, uzio na mifumo ya tahadhari mapema inaweza kuzuia wanyamapori kuingia mashambani na kushambulia mifugo.

Kulinda korido za wanyamapori huruhusu wanyama kusonga kati ya maeneo ya kulisha, kuzaliana na kumwagilia bila kupita katika makazi ya watu.

Mipango ya fidia inaweza kuwasaidia wakulima kurejesha hasara kutokana na uharibifu wa mazao au mashambulizi ya mifugo, kupunguza motisha ya kulipiza kisasi.

Teknolojia kama vile ufuatiliaji wa GPS, mitego ya kamera, ndege zisizo na rubani na taarifa za simu pia zinaweza kusaidia jamii kufuatilia wanyamapori na kupata tahadhari ya mapema.Pale ambapo wanyama huwa tishio kubwa mara kwa mara, mamlaka zinaweza

kutumia hatua stahiki, ikiwa ni pamoja na kuimarisha vikwazo au kuwahamisha wanyama.

Muhimu zaidi, jamii za wenyeji zinahitaji kuhusishwa katika usimamizi wa wanyamapori na kunufaika na uhifadhi.

#