Dollar

42,7117

0.02 %

Euro

50,1553

-0.02 %

Gram Gold

5.962,8900

1.03 %

Quarter Gold

9.698,2800

0 %

Silver

87,0300

2.46 %

Waandamanaji waliobeba mabango na kuimba kaulimbiu za amani walisema sauti ya Afrika lazima isikike kwa nguvu zaidi katika juhudi za kumaliza vita vinavyochochewa na mapambano ya kudhibiti rasilimali za asili.

Matembezi ya amani Mombasa yatoa wito wa kusitishwa kwa vita barani Afrika

Mamia ya wakazi, wanaharakati wa haki za binadamu na wawakilishi wa mashirika ya kijamii walifanya matembezi ya amani katika mji wa pwani wa Mombasa, wakitoa wito wa kusitishwa mara moja kwa vita vinavyoendelea katika mataifa kadhaa ya Afrika, yakiwemo Sudan na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Matembezi hayo, ambayo waandaaji walisema ni ya kwanza ya aina yake jijini humo, yalilenga kuangazia kile walichokitaja kuwa ukimya wa jumuiya ya kimataifa huku vifo vya raia na maafa ya kibinadamu vikiendelea kuongezeka katika maeneo yenye migogoro.

Waandamanaji waliobeba mabango na kuimba kaulimbiu za amani walisema sauti ya Afrika lazima isikike kwa nguvu zaidi katika juhudi za kumaliza vita vinavyochochewa na mapambano ya kudhibiti rasilimali za asili.

“Kile kinachotokea leo Congo au Sudan kinaweza kutokea kwetu kesho, kwa sababu sisi pia tuna rasilimali,” alisema Mwaivu Kaluka, mwanaharakati wa Chama cha Kikomunisti Kenya. “Hivi sio vita vya kikabila tu, bali ni migogoro inayochochewa na watu wenye nguvu wanaopigania rasilimali za Afrika,” aliongeza.

Kaluka alisema mataifa kama Congo na Sudan yana utajiri mkubwa wa rasilimali, lakini wananchi wa kawaida hawafaidiki, akiongeza kuwa uingiliaji wa kigeni umechangia kuendeleza migogoro hiyo.

“Rasilimali za Afrika lazima ziwanufaishe Waafrika,” alisema.

Wito kwa hatua za Kiafrika na kimataifa

Washiriki waliitaka Umoja wa Afrika, jumuiya za kikanda na serikali zenye ushawishi kuongeza juhudi za kidiplomasia na kibinadamu ili kuzuia kupotea kwa maisha zaidi na kuyumba kwa usalama wa kikanda.

Rafik Rauf, muandaaji wa matembezi hayo kutoka shirika la kibinadamu la Marafiki Relief Aid Africa, alisema lengo lilikuwa kuhamasisha uungwaji mkono wa umma na taasisi.

 “Watu wengi sana wanakufa na wengi wanalala njaa,” alisema Rauf. “Matembezi haya yanatusaidia kuhusisha mashirika ya kimataifa, taasisi za Afrika na serikali ya Kenya katika juhudi za kusitisha mapigano na kurejesha amani.”

Wito wa kibinadamu

Sambamba na matembezi hayo, waandaaji waliendelea kukusanya misaada ya kibinadamu ikiwemo fedha taslimu, chakula, maji safi na bidhaa za msingi za usafi, hasa kwa raia waliokumbwa na vita nchini Sudan.

Hisia za kugusa moyo pia zilitolewa na baadhi ya waandamanaji waliotaja mateso ya watoto na wanawake katika maeneo ya vita.

“Kama mama, najiuliza ningejihisi vipi kama hayo yangemkuta mtoto wangu,” alisema Fatma Osman, mmoja wa waandamanaji. “Hatuwezi kufurahia maisha huku wengine wakiuawa na hawana chakula.”

Wasiwasi wa kuyumba kwa usalama wa kikanda

Waandamanaji walionya kuwa kuendelea kwa migogoro barani Afrika kunaweza kusababisha kuyumba kwa usalama hata katika nchi zilizo na amani kwa sasa, na wakatoa wito wa suluhu zinazoongozwa na Waafrika.

Waandaaji walisema matembezi kama hayo yanapangwa kufanyika katika miji mingine nchini Kenya kama sehemu ya kampeni pana ya kuhimiza amani barani Afrika.

Comments

Comment

Comment Your email address will not be published. Required fields are marked*

No comments Yet

#