“Rwanda lazima isimamishe uungaji mkono wake kwa M23 na iondoe wanajeshi wake kutoka mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo,” alisema Waziri wa Hazina wa Marekani, Scott Bessent, katika taarifa yake.
Marekani siku ya Jumatano iliweka vikwazo dhidi ya Wizara ya Ulinzi ya Rwanda kutokana na mgogoro unaoendelea mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo. Hatua hiyo inalenga kuongeza shinikizo kwa serikali ya Rwanda ili kusaidia kukomesha mapigano katika eneo hilo.
“Rwanda lazima isimamishe uungaji mkono wake kwa M23 na iondoe wanajeshi wake kutoka mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo,” alisema Waziri wa Hazina wa Marekani, Scott Bessent, katika taarifa yake.
Rwanda imekana kuliunga mkono kundi hilo lililofahamika hapo awali kama AFC-M23.
Mapigano yanaendelea mashariki mwa Kongo, ambako waasi wanaopigana na jeshi la Kongo na kundi la Democratic Forces for the Liberation of Rwanda (FDLR) wameendelea na operesheni zao. FDLR ni kundi la wanamgambo wa Kihutu wanaohusika katika mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 nchini Rwanda.
Utawala wa Rais wa Marekani, Donald Trump, umekuwa ukijitahidi kupatanisha Rwanda na Congo ili kufikia amani. Nchi hizo mbili zilitia saini makubaliano mwaka 2025 yaliyolenga kumaliza mapigano. Hata hivyo, juhudi hizo hazijaleta mabadiliko makubwa katika hali ya usalama maeneo ya mapigano.
Msemaji wa serikali ya Rwanda, Yolande Makolo, alisema Makubaliano ya Washington yanajumuisha ahadi za kuchukua hatua za kulidhibiti na kuliondoa tishio la FDLR, lakini ahadi hizo hazijatekelezwa.
“Rwanda bado iko tayari kutekeleza kikamilifu Makubaliano ya Washington, ikiwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo iko tayari kutimiza ahadi zake, na mpatanishi akihakikisha kuwa pande zote zinawajibika,” aliongeza Makolo.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Congo imepongeza hatua ya Marekani ya kuiwekea Rwanda vikwazo, ikisema kuwa Rwanda lazima iwajibishwe.
Hata hivyo Waziri wa Mambo ya Nje wa Rwanda, Olivier Nduhungirehe, amesema suala la Wakongo lazima yatatuliwe na Wakongo wenyewe, aliongeza kuwa Rwanda haipaswi kutumiwa kwa yale yanayoendelea nchini Congo.
Alisema hayo katika mahojiano na shirika la habari la AFP pembezoni mwa Mkutano kati ya Urusi na Afrika unaofanyika jijini Moscow.

