Rais huyo wa zamani, mwenye umri wa miaka 64, alisema alifikia uamuzi huo baada ya kura isiyo rasmi iliyopigwa Ijumaa kuonyesha kuwa hakuna hata mmoja kati ya wagombea saba anayeweza kupata uungwaji mkono kamili

Macky Sall wa Senegal ajiondoa katika kuwania nafasi ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa

Rais wa zamani wa Senegal, Macky Sall, amejiondoa katika kinyang'anyiro cha nafasi ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa.

Sall alitangaza kujiondoa kwake kupitia taarifa iliyochapishwa kwenye ukurasa wake rasmi wa Facebook siku ya Jumamosi.

Rais huyo wa zamani, mwenye umri wa miaka 64, alisema alifikia uamuzi huo baada ya kura isiyo rasmi iliyopigwa Ijumaa kuonyesha kuwa hakuna hata mmoja kati ya wagombea saba waliopo kwa sasa anayeweza kupata uungwaji mkono kutoka kwa nchi zote tano wanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa (UNSC).

Wanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama ni Marekani, China, Urusi, Ufaransa, na Uingereza.

Kura hiyo isiyo rasmi pia ilionyesha kuwa Rebeca Grynspan, aliyekuwa Makamu wa Rais wa Pili wa Costa Rica na Katibu Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Biashara na Maendeleo (UNCTAD), ndiye anayeonekana kupendelewa zaidi kumrithi Antonio Guterres wa Ureno katika nafasi ya mkuu wa Umoja wa Mataifa.

Rebeca Grynspan, mwenye umri wa miaka 70, alipokea kura mbili tu za kupinga (veto) kutoka kwa nchi tano wanachama wa kudumu, tofauti na washindani wake wengi ambao walipokea kura nyingi zaidi za kupinga.

Ripoti za vyombo vya habari vya Marekani zinaashiria kuwa Washington inapinga wagombea wote saba walio katika kinyang'anyiro hicho, na iko tayari kuzingatia wagombea wengine ambao wanaweza kuonyesha nia ya kumrithi Guterres.

"Kufuatia kura isiyo rasmi iliyopigwa tarehe 16 Oktoba 2026, kwa ajili ya kuchagua mtu wa kushika nafasi ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, na baada ya kufanya mashauriano na Mheshimiwa Bw. Evariste Ndayishimiye, Rais wa Jamhuri ya Burundi na Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika, pamoja na Mheshimiwa Bassirou Diomaye Diakhar Faye, Rais wa Jamhuri ya Senegal na Mwenyekiti wa ECOWAS, nimeamua kujiondoa katika kinyang'anyiro cha nafasi hiyo," alisema Sall akielezea uamuzi wake wa kujiondoa kwenye kinyang'anyiro cha nafasi hiyo ya juu katika Umoja wa Mataifa.

#