Kipchoge alifafanua upya mipaka ya ustahimilivu wa binadamu. Kuanzia kushinda medali za dhahabu katika Michezo ya Olimpiki hadi kuvunja kikwazo cha kukimbia mbio za marathoni kwa chini ya saa mbili.

Eliud Kipchoge: Gwiji aliyevunja vivkwazo vya kibinadamu vya kukimbia

Huyu ni mtu asiyehitaji kutambulishwa. Eliud Kipchoge, gwiji wa mbio ndefu kutoka Kenya, ambaye alifafanua upya mipaka ya ustahimilivu wa binadamu.

Kuanzia kushinda medali za dhahabu katika Michezo ya Olimpiki hadi kuvunja kikwazo cha kukimbia mbio za marathon kwa muda wa chini ya saa mbili katika tukio maalum, Kipchoge ametumia miaka mingi kuthibitisha kwamba mwanadamu hana mipaka. Katika muendelezo wa makala yetu ya wanariadha wa Afrika, tunamtambulisha Kipchoge.

Lakini ni vipi Kipchoge kutoka vijijini nchini Kenya alifikia hatua ya kuwa mmoja wa wakimbiaji bora wa mbio ndefu (marathon) kuwahi kushuhudiwa duniani?

Akizaliwa Novemba 5, 1984, huko Kapsisiywa katika Kaunti ya Nandi nchini Kenya, Kipchoge alikulia katika mazingira yaliyomlazimu kukimbia kwenda na kurudi shuleni.

Hakutoka katika familia ya wanariadha wa kulipwa; safari yake ilianza na mapenzi ya dhati ya kukimbia,  pamoja na nidhamu iliyomwezesha kugeuza shauku hiyo kuwa taaluma.

Mafanikio yake makubwa ya kwanza yalikuja mwaka wa 2003, akiwa na umri wa miaka 18 tu, aliposhinda taji la dunia la mbio za mita 5,000 jijini Paris, akiwashinda wakali waliokuwa wameshajijengea majina makubwa na kujitambulisha vyema katika ulingo wa kimataifa.

Baadaye alishinda medali ya shaba ya Olimpiki jijini Athens mwaka 2004 na medali ya fedha ya Olimpiki jijini Beijing mwaka wa 2008, kabla ya kuhama kutoka kwenye mbio za uwanjani (track) na kuanza kushiriki mbio ndefu za barabarani (marathon).

Na hapo ndipo alipojijengea sifa na heshima ya kuwa nguli wa mchezo huo.

Kipchoge alishinda mbio za marathon za Olimpiki jijini Rio mwaka wa 2016 na kufanikiwa kutetea taji lake jijini Tokyo mwaka wa 2021, na kuwa mwanamume wa tatu pekee kushinda medali za dhahabu za marathon za Olimpiki mfululizo.

Pia alitawala mbio kuu za marathon katika miji mikubwa, akishinda Berlin, London na Chicago, miongoni mwa mashindano mengine.

Mwaka 2018, aliweka rekodi ya dunia ya marathon ya saa 2:01:39 jijini Berlin, rekodi ambayo aliiboresha hadi saa 2:01:09 mwaka wa 2022.

Kisha ukaja mwaka wa 2019, alipokimbia marathon kwa muda wa chini ya saa mbili jijini Vienna. Muda wake wa saa 1:59:40 ulikuwa wa kihistoria, ingawa haukutambulika kama rekodi rasmi ya dunia kwa sababu tukio hilo lilifanyika chini ya mazingira maalum yaliyodhibitiwa.

Baada ya kipindi chenye changamoto, Kipchoge ameendelea kutafuta malengo mapya zaidi ya medali na rekodi.

Ushindi wake wa hivi karibuni jijini Melbourne, Australia, ni ushindi wake wa kwanza wa marathon katika kipindi cha miaka mitatu, ukikumbusha kuwa bado ana hamu ya kushindana na uwezo wa kuvutia hisia za dunia nzima.

Pia ni kati ya azma yake ya kukimbia marathon katika mabara 7 katika mradi wake wa kuhamasisha dunia juu ya umoja na utangamano.

Kwa Kipchoge, kuvuka mstari haukua mwisho wa safari.

Anafuata falsafa kwamba: “Hakuna binadamu mwenye mipaka.”

Na akiwa na umri wa miaka 41, Eliud Kipchoge bado anaonyesha ulimwengu maana ya maneno hayo.

Tufuatilie TRT Afrika Swahili tunapoangazia vipaji vipya na vinavyochipukia katika riadha barani Afrika ambavyo vinastahili kufuatiliwa.

#