Dollar

43,0636

0.07 %

Euro

50,4409

0.19 %

Gram Gold

6.180,8600

-0.58 %

Quarter Gold

10.390,9600

0 %

Silver

111,0100

-1.31 %

Rais wa Marekani Donald Trump amesifia operesheni ya nchi yake ya kumteka Rais wa venezuela na mkewe, lakini hatua hii imepokelewa kwa shutuma na tahadhari kutoka jamii ya kimataifa kama ukiukaji mkubwa wa sheria za Kimataifa.

Dunia imepokea vipi shambulio la Marekani nchini Venezuela?

Rais wa Marekani Donald Trump bado anaendelea na vitisho vya kuishambulia Venezuela tena.

Kauli ya Trump inakuja baada ya kufanya shambulio la kushtukiza Jumamosi, usiku wa manane na kumteka Rais wa Venezuela Nicolas Maduro na Mke wake Cilia Flores.

Wawili hao, walipelekwa Marekani ambapo wamefunguliwa mashtaka mbali mbali ikiwemo ya ulanguzi wa dawa za kulevya na umiliki wa silaha kwa madai ya kuvuruga amani ya Marekani.

Akizungumzia Operesheni iliyopewa jina ‘Absolute resolve’ Rais wa Marekani Donald Trump aliwasifu wanajeshi wake kwa jinsi walivyofanya shambulio la kijeshi alilosema lilikuwa na ufanisi wa hali ya juu, na kuonesha uwezo wa kijeshi katika historia ya Marekani.

Maduro bado ni Rais

Lakini licha ya yeye mwenyewe kujipongeza, sio wengi waliompongeza au kumuunga mkono kwa hatua hiyo.

Punde tu baada ya tukio hilo, shutuma kali zimeibuka kutoka kwa viongozi mbali mbali duniani wanaoiona hatua hiyo kama ukiukaji mkubwa wa sheria za kimataifa na uingiliaji wa uhuru wa nchi.

Maafisa wakuu katika serikali ya Maduro bado wanaongoza na wametaja kuzuiliwa kwa Maduro na mkewe Cilia Flores kuwa utekaji nyara. Makamu wa Rais Delcy Rodriguez - ambaye pia ni Waziri wa Nishati wa Venezuela ambae anakaimu nafasi ya rais wa muda baada ya kupata baraka za Mahakama Kuu ya Venezuela, anasema Maduro bado anaendelea kuwa rais.

Rodriguez kwa muda mrefu amekuwa akizingatiwa kuwa mwanachama mtendaji katika serikali ya Maduro. Lakini amepinga hadharani madai ya Trump kuwa yuko tayari kufanya kazi na Marekani.

Urusi na China zajitolea kushirikiana na Venezuela

Ndani ya Venezuela na nje kumekuwa na maandamano mbali mbali, wengine wakipinga hatua hiyo ya Marekani huku baadhi wakiunga mkono, wachambuzi wanasema wengi wa wanaounga mkono ni raia wa Venezuela wanaoishi nje ya nchi.

Uhispania na nchi tano za Amerika Kusini - Brazil, Chile, Colombia, Mexico, na Uruguay - zimeelezea wasiwasi mkubwa baada ya operesheni hiyo ya Marekani, na kuonya juu ya hatari kwa usalama na utulivu wa kikanda.

Uhispania ndiyo ilikuwa mkoloni wa mataifa hayo.

Rais wa Urusi Vladmir Putin na mwenzake wa China Xi Xinping walishutumu shambulio hilo la Marekani huku wakitangaza utayari wao kushirikiana na watu wa Venezuela.

Trump ni kama sikio la kufa

Afrika Kusini ilipinga waziwazi pia shambulio hilo na kutoa wito kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kutoa kauli ya pamoja ya kulaani uvamizi huo.

Iran ilisema shambulio hilo ni ukiukaji wa haki ya kimataifa na uhuru wa kujitawala.

Ufaransa pia ilisema huo ni ukiukaji wa sheria za kimataifa.Pia jumuiya ya kimataifa imeshutumu ikiwemo Umoja wa Afrika. EU imeelezea wasiwasi lakini haikushutumu moja kwa moja japo imetoa wito wa kuheshimiwa kwa sheria za kimataifa.

Trump  sasa amekuwa kama sikio la kufa, mbali na uvamizi huo, bado anatishia kuishambulia tena Venezuela iwapo utawala wa muda wa nchi hiyo hautatimiza maagizo yake.  Vitisho hivyo vimekwenda mbali zaidi, kwani ametishia pia kuishambulia Mexico, Cuba na Colombia.

Comments

Comment

Comment Your email address will not be published. Required fields are marked*

No comments Yet

#